Sambaza....

Kocha mkuu wa timu ya Soka ya Gor Mahia ya nchini Kenya Daylan Kerr amesema wachezaji wake walicheza vizuri katika mazingira magumu nchini Algeria dhidi ya USM Alger hadi kupelekea kupoteza kwa mabao 2-1.

Kerr ambaye timu yake imeshindwa kuweka historia ya pekee kwa Kufuzu kwenye robo fainali ya kombe la shirikisho baada ya kichapo hicho amesema kucheza katika nchi za Kaskazini hasa katika kipindi muhimu kama kile ilikuwa ni ngumu kuweza kupata ushindi.

Amesema hawaamini kama wamefika Kenya salama hasa ukizingatia mazingira magumu ambayo walipitia ya Kabla na wakati wa mchezo lakini amewaomba radhi mashabiki wote kwa kushindwa kufuzu hatua ya robo fainali.

Daylan Kerr, akiwa na wachezaji wake

“Tulijitolea Kwa nguvu zote kwenye ile mechi, nawapongeza wachezaji wangu, tulijua kucheza na timu za Afrika Kaskazini kwa wakati muhimu kama ule ni ngumu sana, kwanza hata tunashukuru tumefika hapa salama,” Kerr mzaliwa wa Malta amesema.

Kocha huyo ambaye ameisadia Gor Mahia kutwaa taji la 17 la ligi kuu nchini Kenya amesema kwa sasa wanajiandaa na mchezo wa FA ‘SportPesa Shield’ hatua ya Robo fainali Jumamosi dhidi ya Kariobangi Sharks katika uwanja wa Machakos.

Mabingwa hao mara 10 wa taji hilo wamekaa na ukame wa takribani miaka sita, Kwani Mara ya mwisho kutwaa taji hilo ilikuwa Mwaka 2012.

Sambaza....