Sambaza....

 

Aliwah kujibebea mashabiki wengi sana hapa nchini kulingana na aina ya soka ambalo aliwahi kulionesha kwenye ligi yetu hii.

Kipindi anaingia aliingia na mfumo ambao ulionekana mgeni sana kwenye ligi yetu, lakini ndiyo mfumo ambao ulikuwepo sokoni kwa kipindi hicho.

Mfumo ambao ulikuwa unaendana na mabadiliko ya sasa ya mpira wa miguu. Mfumo wa kutumia mabeki watatu.

Mfumo ambao , Masoud Djuma alifanikiwa kutengeneza Simba ya kuvutia na ya kutisha. Ilitisha sana, na ilivutia sana kila ilipokuwa inacheza.

Furaha ya mashabiki wa Simba ilikuwa ni kuiona timu yao ikifanikiwa kushinda ushindi ambao ulikuwa unaonekana ushindi mkubwa tena ikiwa inacheza soka la kuvutia.

Hii ndiyo ilikuwa furaha kubwa ya mashabiki wa Simba na ndiyo silaha kubwa kwa kocha yeyote kuitumia ili kushika hisia za mashabiki wa Simba.

Hakikisha timu inacheza soka la kuvutia huku ikishinda kwa idadi kubwa ya magoli, hapo ndipo utafanikiwa kuingia kwenye mioyo ya mashabiki wa Simba.

Hapa ndipo alipofanikiwa Masoud Djuma, aliwatia ukichaa mashabiki wa Simba, aliwafanya wamwamini yeye ndiye mtu sahihi pekee katika timu ya Simba.

Aliwafanya waamini kuwa Simba iliumbwa kwa ajili ya kufundishwa na kocha mmoja naye ni Masoud Djuma. Na kibaya zaidi mfumo ule wa 3-5-2 ndiyo uliwatia ukichaa kabisa.

Waliona ni kitu kipya na sahihi kabisa katika timu ya Simba. Kwa kifupi walimwamini sana Masoud Djuma.

Wengi walikuwa tayari kumuunga mkono kwenye kila hali kwa sababu waliamini yeye ndiye Masia ambaye amekuja kuwaokoa kwenye mateso.

Walichoka sana kukaa kwenye mateso ya kunyanyaswa na Yanga kila mwaka. Yanga walijiwekea hatimiliki ya kuchukua ligi.

Haya maisha waliyachoka sana mashabiki wa Simba, walitaka kuishi kwenye maisha mapya, maisha ambayo yamejaa furaha kila siku.

Maisha ambayo yangewawezesha wao kunywa chai yenye asali, mboga iliyoungiwa asali, wali ulioungiwa asali, hata maji ya kunywa walitamani kutumia asali.

Kwao wao walitaka maisha ya pepo, walitamani hata kuogea asali tu. Hawakutaka mateso kabisa ndani ya nafsi zao.

Haya ndiyo maisha ya shabiki yeyote duniani. Hakuna shabiki ambaye amewahi kuridhika na matokeo mabovu.

Hakuna shabiki ambaye amewahi kufanikiwa kuwa na moyo wa uvumilivu kabisa. Neno uvumilivu kwao liko mbali sana na mioyo yao.

Ndiyo maana walichoka kuwaona Yanga wakibeba ligi kuu wao tu. Hawakuwa na uvumilivu kabisa kwenye hilo.

Masoud Djuma alipokuja kuwaletea ladha tofauti, ladha ambayo ilisababisha wao wabebe mpaka ligi kuu ya Tanzania bara, walimuona yeye ndiye mwokozi wao.

Ulikuwa na uwezo wa kuwaambia nini mashabiki wa Simba mbele ya Maoud Djuma ?, kwa Masoud Djuma , mashabiki wa Simba macho yao yalikuwa na upofu na masikio yao yalikuwa na ukiziwi.

Ndiyo maana hata Pierre Lenchantre aliondoka na kumuacha Masoud Djuma. Hata Patrick Assumes alipokuja kidogo aondoke ili amwache Masoud Djuma.

Isingekuwa busara za viongozi wa Simba, Masoud Djuma alikuwa anabaki na Patrick Assumes alikuwa anaondoka.

Na hii ni kwa sababu , Masoud Djuma alikuwa amejipenyeza kwenye mioyo ya mashabiki wa Simba.

Ndiyo maana tulishuhudia kocha mkuu wa Simba alirushiwa chupa cha maji pale Mwanza. Mashabiki waliona kuwa yeye ndiye alikuwa sababu kubwa ya Simba kupata matokeo mabovu.

Na walimuona Masoud Djuma ndiye Musa anbaye angeweza kuwavusha kwenda Kaanani. Hawakutaka kabisa kumpa muda Patrick Assumes.

Hawakutaka kabisa kumwamini na kumwelewa. Lakini baada ya Masoud Djuma kuondoka , Patrick amefanikiwa kutengeneza Simba inayotisha kuzidi ile iliyokuwa chini ya Masoud Djuma

Sambaza....