Kiungo wa timu ya Taifa ya Tanzania “Taifa Stars” na Zanzibar “Zanzibar Heroes” amesema moja ya sababu zinazomuondoa Yanga ni manyanyaso na pia kuongezewa mkataba wa mwaka mmoja bila yeye kujua kisa tu mkataba uliandikwa kwa Kiingereza.
Feisal akiongea katika kipindi cha asubuhi cha Clouds fm anakiri Yanga walikiuka makubaliano ya kimkataba waliyokubaliana kwa mdomo na kumpa mkataba tofauti.
“Shida yangu Yanga ni manyanyaso si mshahara, nilisaini nkataba wa miaka miwili kumbe yeye kiongozi aliongeza mwaka mmoja bila ridhaa yangu, mkataba uliandikwa kwa Kiingereza,” alisema Feisal na kuongeza
“Fedha ya usajili tulikubaliana Tsh. Milioni 100 kwa pamoja, pia si kweli walinipa fedha yote, nilipomaliza kusaini mkataba waliniingizia Tsh. Milioni 10 tofauti na tulivyokubaliana, ikaenda hivyo kupewa hela mpaka tugombane ndio wananipa kimafungumafungu.”
Aidha Feisal pia amesema hawezi tena kurudi Yanga kwani hana uhuru tena na hafurahii kufanya kazi na Wananchi hivyo ni vyema akaruhusiwa kuondoka zake akacheze sehemu nyingine.
“Kuna wakati niliambiwa nauza mechi na baadhi ya viongozi wa Yanga. Siwezi kurudi Yanga kwa sasa kwa kuwa ninahitaji kucheza na kufanya kazi nikiwa huru,” alimalizia Feisal.