Klabu ya soka ya Yanga imefanya usajili kwa wachezaji watano pekee na wote wakiwa wakigeni wakienda kuungana na wale walikuepo msimu uliomalizika.
Yanga imemsajili Benard Morisson, Joyce Lomalisa, Lazarious Kambole, Gael Bigirimana na Aziz Ki mpaka sasa.
Achana na wote hao twende kwenye usajili wa Aziz Ki akitokea Asec Mimosa kwenda Yanga, usajili ambao unatajwa kuwa wa gharama zaidi Yanga na nchini kwa ujumla.
Ki kiasili ni kiungo mshambuliaji mwenye uwezo wa kucheza winga zote mbili au nyuma ya mshambuliaji, lakini hufanya vyema zaidi akicheza kama namba kumi yaani nyuma ya mshambuliaji wa mwisho.
Katika mchezo wa kilele cha Wiki ya Wananchi dhidi ya Vipers Feisal alianza kama namba kumi nyuma ya Makambo nafasi ambayo hucheza siku zote tangu Kocha Nabi alipopewa mikoba yakuinoa Yanga.
Kipindi cha pili Yanga ilifanya mabadiliko na Aziz Ki aliingia uwanjani kuchukua nafasi ya Nkane ambae alianza kama winga, baada ya mabadiliko hayo Aziz Ki alicheza kama dakika tano akitokea pembeni upande wa kulia halafu baadae akaingia kati kucheza nyumba ya mshambuliaji Fiston Mayele.
Mabadiliko hayo yalimfanya Fei kusogea pembeni kucheza kama winga wa kulia kabla yakutolewa na dakika za mwishoni. Ki alicheza namba kumi huku akionekana kufurahia zaidi mchezo na eneo hilo kwa kiasi kikubwa.
Licha ya kutokucheza vyema katika mchezo ule lakini pasi na shaka huenda Nabi akaamua kumtumia katika eneo hilo.
Kwa vyovyote vile kama Nabi ataamua kwenda na mfumo wa 4:2:3:1 huenda kuna mabadiliko ya upangaji timu yakamuathiri Feisal Salum. Kama mawinga wa Yanga wakiongozwa na Benard Morrison, Jesus Moloko, Denis Nkane na Dickson Ambundo huenda mwalimu akaamua kumtumia Azik Ki kama namba kumi kama ambavyo alimalizia katika mchezo dhidi ya Vipers.
Kama Ki atakua na wakati mzuri na mwalimu Nabi akafurahishwa na jinsi ambavyo mawinga wake wanavyocheza ni wazi Feisal atapata mshindani mpya katika eneo lake na kumfanya kugombea namba na Aziz Ki.
Kazi ni kwake Feisal kutetea nafasi yake na kumbishia Aziz Ki kwa kumshawishi Professor Nabi aendelee kumpanga katika eneo la kiungo wa kati nyuma ya ushambuliaji.