Ligi ya Championship (zamani Ligi daraja la kwanza) imeshika kasi na mwishoni mwa wiki hii itaendelea huku mchezo kati ya Pamba Fc na Kitayosce Fc ukiwa ndio mchezo wakuvutia na unaofwatiliwa zaidi.
Pamba mwenye alama 47 wapo nafasi ya tatu watakua nyumbani wakiwakaribisha Kitayosce wanaoshika nafasi ya pili wakiwa na alama zao 49 katika mchezo unaotegemewa kuwa wa ushindani na mkali kwelikweli utakaopigwa katika uwanja wa Nyamagana Mwanza Jumamosi hii sa kumi jioni.
Kuelekea mchezo huo muhimu kwa Pamba tayari wiki yote kumekua na kampeni kubwa ya kuhamasisha mashabiki wajitokeze kwa wingi ili kuiunga mkono timu yao kuelekea mchezo huo muhimu.
Kuelekea mchezo huo tayari Mkuu wa mkoa wa Mwanza Adam Malima ameingilia kati na kuipa nguvu Pamba ili iweze kurejea Ligi Kuu kwa kununua tiketi 500 ili mashabiki waingie kuishangilia timu yao.
“Tayari nimechangia Tiketi 500 kwaajili ya mashabiki wa wana Mwanza kuja kuishangilia pamba na tunaendelea kuwashawishi wadau wengine kuchangia ili kuleta hamasa zaidi.
Tunahitaji watu wajae katika uwanja wa Nyamagana tulitamani kwa ukubwa na umuhimu wa mechi tungecheza hata Kirumba lakini tumechelewa,” Adam Malima alisema
Mkuu huyo wa mkoa amesema mchezo huo ni wa muhimu sana kutokana na msimamo wa Ligi ulivyo hivyo ni lazima washinde mchezo huo na vyema mashabiki wakaujaza uwanja mapema.
Adam Malima “Mchezo wa Jumamosi Dhidi ya Kitayosce FC ni mchezo ambao lazima tushinde na niwaombe wapenzi na wananchi wa mkoa wa Mwanza waje mapema katika uwanja wa Nyamagana ili kufika Saa 9:00 Alasiri Uwanja uwe umejaa”
Michezo mingine katika Ligi hiyo itakayopigwa mwishoni mwa wiki hii ambayo pia itakua mubashara kupitia TV3 katika king’amuzi cha Startimes ni kati ya Mbeya Kwanza na Green Worriers, Fountaine Gate vs African Sports, JKT Tanzania na Mbuni Fc, michezo yote hiyo itapigwa Jumamosi.
Pia Jumapili Ken Gold watawakaribisha Ndanda wakati Biashara watakua nyumbani dhidi ya Transit Camp. Na Jumatatu kutakua na mchezo mmoja pekee ambapo Pan Africa watawakaribisha Copco Fc.