Mshambuliaji wa zamani wa Real Madrid na AC Milan Antonio Cassano ametangaza kustaafu soka kwa mara ya tatu, siku chache tu baada ya kurejea uwanjani.
Cassano ambaye aliwahi kuichezea timu ya Taifa ya Italy amesema sasa ameamua kabisa kuacha na soka kwa muda wa kufanya hivyo umefika baada ya siku chache tu aliporudi uwanjani kuitumikia timu ya Virtus Entella inayoshiriki Serie C.
“Ile siku imefika, siku ambayo unaamua kwamba kila kitu kimefika mwisho, kwa siku kadhaa hapo nyuma nilikuwa kwenye mazoezi, na kugundua kuwa sina tena nguvu za kuendelea kufanya mazoezi,” amesema Cassano mwenye umri wa miaka 36.
Mechi ya mwisho ya ushindani kwa Cassano aliichezea Sampdoria mwezi mei mwaka 2016 na alitangaza kurejea uwanjani mwaka 2017 akiwa na Hellas Verona lakini hazikupita siku nyingi akatangaza kustaafu lakini baadae alibadilisha maamuzi na kurejea ambapo alicheza michezo miwili ya kirafiki na timu hiyo kabla ya kutangaza kustaafu kwa mara nyingine.
“Ili uweze kucheza mpira unatakiwa kuwa na shauku na kipaji, lakini zaidi ya yote kujitoa na muda huu nina vipaumbele vingine,” amesema.
Cassano ameichezea timu ya Taifa ya Itali michezo 39 kati ya mwaka 2003 na 2014, akiwa Real Madri aliweza kutwaa taji la LaLiga sambasamba na kunyakuwa taji la Serie A akiwa na AC Milan.