Mkoa wa Kigoma unatarajia kushuhudia burudani kubwa ya soka baada ya zaidi ya miaka 20, Pale ambapo mabingwa wa kihistoria Yanga watakapocheza mchezo wa kirafiki na Singida United kutoka mkoani Singida.
Mkurugenzi wa Singida United Festo Richard Sanga amesema mchezo huo ambao utapigwa katika uwanja wa Lake Tanganyika, Septemba 05, 2018 ni sehemu ya maandalizi ya ligi kuu soka Tanzania bara kipindi ambapo ligi itakuwa imesimama kupisha majukumu kwa timu ya Taifa.
Sanga amesema mchezo huo umenuia katika kuamsha ari ya michezo katika kanda ya mikoa ya Magharibi na hasa Kigoma ambapo kwa muda mrefu umekosa hamasa huku ukiendelea kutoa nyota wengi wanaowika hata sasa.
“Huu mchezo umenuia kuamsha ari ya michezo katika mkoa wa Kigoma, kama unakumbuka mkoa huu umepata kuwika sana ukileta wachezaji mashuhuri, lakini umekuwa hauna timu ya ligi kuu kwa muda mrefu,”
Sanga amesema maandalizi ya mchezo huo yanaendelea vizuri na wamejipanga kuhakikisha wanawaburudisha wakazi wa Kigoma na maeneo ya jirani ambao wamekuwa na kiu ya muda mrefu kutazama timu kubwa zikicheza.
Aidha Sanga amesema mbali na mchezo huo pia wanatarajia kusafiri tena hadi mkoani Rukwa ambapo wakiwa hapo watacheza mchezo mwingine wa kirafiki na Yanga siku ya Septemba 8 katika mji wa Sumbawanga.
Kwasasa Singida United ipo mkoani Singida wakijiandaa na mchezo wa ligi dhidi ya Wabishi Mbao FC ili hali Yanga wao wapo nchini Rwanda wakijiandaa na mchezo wa mwisho wa kundi D kombe la shirikisho Afrika dhidi Rayon Sports siku Jumatano.