Sambaza....

Wengi wameyazungumza haya ya kwamba Yanga ni timu ya kawaida lakini hali inakuwa tofauti hasa pale dakika 90 zinapokamilika, lakini inaonekana kama Biashara United ya Mara wamedhamiria kudhihirisha hili.

Meneja wa Biashara United Amani Richard Josiah amesema kikosi chao kinataka kuonesha hilo kuwa Yanga ni timu ya kawaida pale watakapokutana katika mchezo wa ligi Disemba tisa Jijini Dar es Salaam kwenye uwanja wa Taifa.

Amani amesema kikosi kipo Dar toka Jumanne na wamekuwa wakifanya Mazoezi ya mwili na akili kuwajenga wachezaji wake kabla ya mchezo huo ambao yeye ameutaja Kama mchezo wa kuonesha udhaifu wa Yanga na kuitangaza Biashara United.

“Kwetu sisi hatuendi kujaribu bali tumekuja kuwafunga Yanga kwasababu Yanga kwa sasa haina kikosi bora, Wachezaji wenywe wanataka kuweka historia kwa kuifunga Yanga na kuondoa rekodi yao ya kutofungwa,” amesema.

“Yanga ni timu kubwa na pia ni timu ambayo haitabiriki kabisa, lakini sisi tumekuja kupata matokeo mazuri na najua tukiifunga Yanga tutajitangaza…Licha ya kupoteza mechi za nyuma lakin sisi tumejipanga kuweka historia hapa Dar es Salaam tunakwenda uwanjani kusaka pointi tatu, sisi tutawajenga wachezaji wetu kisaikolojia na kuwaambia ni kitu gani tunatafuta,” ameongeza Amani.

Kwa sasa Biashara United ambayo awali ilikuwa ikitambulika kama Polisi Mara, wapo mkiani Kabisa mwa msimamo wa Ligi wakiwa na alama 10 baada ya kucheza michezo 14, kati ya hiyo wameshinda mchezo mmoja pekee dhidi ya Singida United.

Sambaza....