Katika kipindi hiki ambacho timu mbalimbali zinatafuta wachezaji mbalimbali ili kuimarisha vikosi vyao kwa ajili ya msimu ujao , tetesi zimekuwa nyingi sana ambazo zimekuwa zikihusisha wachezaji mbalimbali na vilabu mbalimbali.
Moja ya taarifa ambayo inazidi kuenea na habari ya beki wa KCB ya Kenya kutakiwa na klabu ya Simba ambao ni mabingwa watetezi wa ligi kuu nchini Tanzania.
Habari zinadai kuwa Simba imekuwa katika mbio za kutaka kumsajili beki huyo kisiki wa kati ambaye anazidi kufanya vizuri katika ligi kuu ya Kenya akiwa na klabu ya KCB ambaye ni Michael Kibwate.
Michael Kibwate amekuwa kwenye kiwango kizuri msimu huu wa ligi ambayo imesimama kutokana na ugonjwa wa Covid-19. Kiwango cha Michael Kibwate kimekuwa kikizivutia vilabu vingi Kenya na hapa Tanzania hasa hasa Simba.
Akizungumza na mtandao huu wa Kandanda.co.tz kuhusu taarifa za yeye kutakiwa na Simba amedai kuwa kwa sasa siyo taarifa rasmi kama ambavyo watu wengi wamekuwa wakisema.
“Taarifa za mimi kutakiwa na klabu ya Simba kwa sasa siyo taarifa rasmi , na siwezi kuzungumza zaidi kwa sababu siyo taarifa rasmi nazisikia tu kama ambavyo wewe unavyozisikia”- alisema Michael Kibwate.
Michael Kibwate alipoulizwa kuhusu yeye kama yuko tayari kucheza katika klabu hiyo ya Simba ,amedai kuwa kwa sasa anatamani sana kucheza ligi kuu ya Tanzania hivo ikija ofa atakubali.
“Kwa sasa hakuna ofa ambayo imeletwa ila kama kutakuwepo na ofa basi Mimi nitakubali kuichukua kwa sababu mpaka sasa hivi natamani kucheza katika ligi kuu ya Tanzania hasa hasa klabu ya Simba”- alimalizia Michael Kibwate