Sambaza....

Inatajwa kuwa ni miongoni mwa mechi zenye mvuto zaidi Afrika Mashariki. Hii ni zaidi ya “derby” kwa Tanzania, kila mtu huacha kazi zake kwa muda wa dakika tisini kupisha mechi hii ichezwe.

Maandalizi ya mchezo huu huchukua zaidi ya wiki mbili, yaani timu huwa katika presha kubwa na kila moja ikitaka kupata matokeo. uwanja wa taifa umegawanywa kwa kigezo cha mashabiki, yaani kuna upande wa mashabiki wa Yanga na wa Simba hata kwa mechi za kawaida, hapo ndipo utakapobaini kwanini hii ni “derby”.

Zichezapo Simba na Yanga, Tanzania na Afrika mashariki husimama kwa muda, ndio maana “derby” hii inatajwa kuwa ni derby ya 5 kwa ukubwa Afrika, yaani baada ya Orlando Pirates vs Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, Raja Casablanca vs Athletic Club ya Morocco, Al Ahly vs Zamalek ya Misri, Club Africain vs Sportive de Tunis ya Tunisia, kisha inafuata KARIAKOO DERBY.

Mzuka wa mechi hii, huwa hauathiriwi na hali ya uchumi ya klabu husika wala matokeo. Timu hizi ni watani wa jadi, hivyo haijalishi timu moja ipo katika hali gani, lakini presha na ukubwa wa mchezo ni uleule.

Mechi ya mwisho katika mzunguuko wa kwanza, Simba akimkaribisha Yanga, iliisha kwa sare tasa huku timu zote zikionekana kukamiana vya kutosha.

Sasa ni mzunguuko wa pili, timu zote zina makocha wale wale waliosimamia derby ya kwanza, Simba wakiwa na Patrick Aussems na Yanga wakiwa na Mwinyi Zahera akikaa katika benchi kwa mara ya kwanza kama kocha wa Yanga. Mchezo wa kwanza, Simba ilitawala mpira kwa kiasi kubwa, na ndio timu iliyoingia katika mchezo huo ikiwa na matumaini makubwa ya kupata ushindi lakini mambo yakawa ndivyo sivyo.

Kwa sasa, Yanga inaongoza ligi ikiwa na alama 58 ikicheza michezo 23, Simba ipo katika nafasi ya nne ikiwa na alama 36, ikicheza mechi 15 pekee. Yanga itaingia na mzuka kutoka na kuongoza ligi, huku Simba ikiingia kwa kujiamini zaidi baada ya kuifunga Al Ahly ya Misri katika mashindano ya Klabu bingwa Afrika.

Kwa jinsi timu zote zinavyocheza na aina ya wachezaji waliokuwa nao, hakika itakuwa ni derby ya “kufa mtu” yaani natarajia nyasi za uwanja wa taifa kuchakaa. Kuna maeneo mengi yatadhihirisha kuwa Simba na Yanga ni “derby” kubwa Afrika na kwa wachezaji pia.

Kandanda.co.tz inakuletea “battle” nane zitakazo shuhudiwa kwenye derby hii. Wachezaji watakwaana, watapambana na kupimana kwa vitu vingi, uwezo wa kumiliki mpira, nguvu, kufunga na kiwango cha mchezaji binafsi kutokana na “game plan” ya mwalimu. Acha nikupe battle zenyewe sasa, kuanzia kwa walimu wenyewe;

  1. Mwinyi Zahera vs Patrick Aussems (Falsafa na mifumo).

Hakika patachimbika! Makocha wote wawili wanaonekana kuwa na muendelezo (consistency) wa aina Fulani ya soka. Nikianza na Mwinyi Zahera, soka lake haliko mbali na falsafa ya Yanga kwa kipindi kirefu sasa yaani kushambulia kupitia pembeni.

Aussems

 Mabeki wa pembeni hutumika kupandisha mashambulizi wakisaidiana na viungo wa pembeni, yaani Gadiel Michael na Pius Buswita au Matheo Anthony husimama upande wa kushoto, Paul Godfrey na Mrisho Ngasa husimama upande wa kulia, kusaidiana kupandisha mashambulizi na kulinda.

Ni mara chache kwa kocha Zahera kuvunja winga ya kushoto na kumuweka mshambuliaji, na hapo ndipo Hamis Tambwe na Heriether Makambo hucheza  pamoja. Aina ya mipira wanayocheza huwa ni mirefu kuelekea pembeni na katikatika. Mipira hii mirefu huanzia kwa mabeki wa kati, Kelvin Yondani na Dante.

Kuthibitisha falsafa hii, yatazame magoli mengi ya Yanga ni ya krosi za mabeki wa pembeni au mawinga, zilizodondoshwa katika sita ya mpinzani na hapo ndipo, Makambo au Tambwe utawaona wabaya kutumia vichwa kufunga magoli.

Zahera Mwinyi

Kwa upande wake, Patrick Aussems hushambulia kupitia pande zote, lakini eneo muhimu kwake kupatia magoli ni eneo la kati. Simba huwa haina mawinga kama ilivyo kwa Yanga. Simba ina viungo wa kati wanaopitia pembeni, mabeki wa pembeni hutumika kama mawinga kwa muda wote.

Eneo lake la ushambuliaji, huwa na washambuliaji watatu kwa wakati mmoja, Meddie Kagere, Emmanuel Okwi na John Bocco. Katika mechi zenye ushindani zaidi huu ndio mfumo anaoutumia ukilinganisha na mechi za kawaida ambapo humpa nafasi ya Rashid Juma kucheza kama Winga kwa lengo maalumu hasa akiona timu pinzani inatumia upande Fulani kama muhimili wa mashambulizi yake.

Aina ya soka wanalocheza ni pasi fupi fupi, mara chache hupiga pasi ndefu zenye uhitaji. Pasi hizo huanzia kwa beki, Paschal Wawa na kiungo Jonas Mkude. Hivi vyote vinaunganishwa na mfumo wa 4-3-3 au 4-4-2. Mifumo hii imeonekana kuibeba Simba kutokana na aina ya wachezaji waliopo.

Bila shaka, kuna uwezekano wa Yanga kuanza na mshambuliaji mmoja, yaani 4-5-1 huku wakitegemea mawinga na mabeki kushambulia kupitia pembeni, wataweka viungo watano katikati ili kushusha presha ya Simba kumiliki mpira na kutengeneza nafasi nyingi za magoli. Hivyo ni 4-3-3/4-2-2 pasi fupifupi  vs 4-5-1/4-4-2 pasi ndefu kupitia pembeni.

2.Emmanuel Okwi  vs Gadiel Michael Kamagi.

Usipime! Gadiel  huenda atakuwa na kibarua kigumu kumzuia Okwi ambaye anaonekana kuwa moto kwa mechi za hivi karibuni. Katika mechi dhidi ya Al ahly, Okwi alicheza namba 7 katika kipindi cha pili kwenda kuzima mashambulizi kutoka kwa beki wa kushoto  na alifanikiwa kwa kiwango kikubwa.

Okwi

Kama Okwi atapangwa tena katika eneo hilo basi mpinzani wake wa kwanza atakuwa beki wa kushoto, Gadiel  na atamzuia kushambulia kupitia pembeni. Okwi ana kasi  na uwezo mkubwa wa kukimbia na mpira, kupiga vyenga, si mchezaji wa kumuacha kwa hatua hata moja, ana kasi anapolitazama lango la mpinzani, ni mzuri kupiga mashuti hata nje ya 18.

Gadiel atakuwa na kazi kubwa moja nayo ni kuhakikisha, Okwi hatembei, hapigi krosi wala kupiga shuti langoni. Jukumu kubwa ni kuzuia uzoefu wa Mganda huyo usilete madhara katika lango la Yanga huku akifanya mpango wa kushambulia kupitia pembeni.

Gadiel Michael

Kwa jinsi ilivyo, kama Okwi atacheza namba 7, basi natarajia Gadiel kutotumika kama ilivyozoeleka, yaani hatoshambulia kwa sababu Okwi hufanya jukumu la ulinzi  kuanzia juu, pia hatari ya kushambulia na kumuacha mchezaji mwenye kasi kama Okwi ni sawa na kumkimbiza mwizi wakati umeacha mlango wazi.

         3.Ibrahim Ajib vs James Kotei.

Ni aina nyingine ya mpambano, kiungo mshambuliaji dhidi ya kiungo mkabaji. Ajib yeye ni namba 10 ya kisasa, inayocheza kama kiungo mshambuliaji. Hakuna anayetilia shaka uwezo wake wa kufunga mabao dhahabu, upigaji wa mipira ya adhabu, vyenga na umiliki wa mpira kwa ujumla.

Ajib

Ajib ana macho ya mwewe, anapiga pasi za kila aina, anajua kutengeza “assist”. Kiufupi Ajib ni mpishi, na kuna wakati anakuwa mlaji. Pale Simba kutakuwa na James Kotei.

James Kotei, ni “stopper” huzuia pasi mpenyezo, si rahisi kumpita mkikutana uso kwa uso “man to man” hakubali kushindwa kirahisi. Ni aina ya viungo wakabaji wa kisasa kabisa, akichagizwa na matumizi ya nguvu na “undava”.

Ajibu atakuwa na jukumu moja kabla ya kutimiza la pili, kwanza ni kumpita James Kotei kabla ya kupiga pasi ya mwisho au kupiga shuti. Ajibu anaweza akatumia faida ya utukutu wa Kotei kupata faulo za kupiga, na kama tunavyomjua Ajibu, nafasi hizo kwake ni kama dhahabu. Natarajia kuiona vita hii ya aina yake.

4.Jonas Mkude vs Papy Tshishimbi/ Feisal Salum “Fei Toto”.

Kwanini pasichimbike pale kati? Nani yupo tayari kukosa mchuano na mtifuano huu wa viungo pale taifa? Hili ni battle. Tshishimbi na Feisal ni viungo wawili wanaocheza eneo la kati, wote wakibadilishana majukumu, yaani Tshishimbi akiwa kiungo mshambuliaji, basi Feisal hubaki chini yake kama “Holding Midfielder” hufanya hivyo kwa dakika zote wakicheza pamoja.

Kutakuwa na kibarua kizito katika kubadilishana majukumu hayo kwakuwa, pale Simba kuna kiungo mwenye uwezo mkubwa kumiliki mpira, ana nguvu miguuni, stamina kubwa na uwezo wa kupiga pasi za mwisho na kupiga mashuti naye si mwingine ni Jonas Mkude.

Papy

Mkude atakuwa kikwazo kikubwa kwa viungo hawa wawili kubadilishana majukumu  hasa katika kipindi cha mpito (mabadilishano) hapo ndio hutoka upenyo kwa mkude kutawala eneo la kati. Mkude naye atakuwa na jukumu zito la kuwakaba (marking)  wachezaji hawa wawili japo kiasili Feisal hatumii nguvu kubwa sana kupokonya mipira na kukaba ndio maana itakuwa ni vita kwani atakutana na mkude anayetumia nguvu na stamina kubwa, na uwezo wake wa kupiga pasi.

Eneo hili la viungo lina watu wenye uwezo wa kupiga mashuti wakiwa nje ya 18. Magoli mawili ya Feisal hivi karibuni yanathibitisha ninachokwambia. Usisahau Simba kuna Jonas Mkude, naye siku hizi anapiga mashuti nje ya 18. Je ni nani kumzuia mwenzake kupiga shuti? Jumamosi sio mbali.

5.Pius Buswita/ Matheo Antony  vs Zana Oumary Coulibaly.

Ni vita ya kiberenge dhidi ya beki wa kulia. Akianza Buswita au Matheo yote heri, wachezaji wote wawili ni wazuri kushambulia kwa kasi kupitia pembeni. Kasi ya Buswita huenda ikawa tishio kwa Coulibaly.

Kama mwalimu Aussems atamuanzisha Coulibaly basi itakuwa ni miongoni mwa battle za maana kabisa katika Kariakoo derby. Coulibaly ameonyesha kiwango poa katika mechi za hivi karibu, lakini bado ni mzito hasa katika kurudi haraka baada ya kwenda kushambulia.

Zana Coulibaly

Uzito wa Coulibaly utawasaidia mawinga wa pembeni hasa kwa mashumbulizi ya haraka “counter attack”. Yanga hutumia mipira mirefu katika kushambulia, inahitaji beki mwenye kasi kubwa kumzuia winga mwenye kasi kubwa pia wakati wa kushambulia ambapo kitu hiki amekosa Coulibaly.

Kwa mantiki hiyo sitarajii, Coulibaly atatumika sana katika kushambulia kupitia pembeni badala yake atabaki nyuma kulinda na huenda akashambulia lakini akipata nafasi ya wazi ya kufanya hivyo. Kama Coulibaly ataamua kujilipua basi madhara yatabaki kwa Simba.

6. Meddie Kagere Vs Andrew Vicent/Yondani.

Wote tunasubiri kuona kile kitakachotokea hasa kwa mabeki wawili Dante na Yondan dhidi ya Kagere na Bocco. Kwa sasa Kagere na Bocco wanaonekana kuwa “unstoppable” watakutana na ukuta wa Mererani kule Arusha. Ni vita ya nguvu, undava na maneno!…

Kagere, ndio mfungaji bora kwa Simba kwa sasa, ligi kuu na klabu bingwa, ana nguvu za miguu, mashuti yake ni mazito na yanakidhi haja. Yuko taratibu lakini humiliki mpira kwa kutumia nguvu za mbavu zake, huhitaji nafasi ndogo sana kupiga shuti kali langoni, miguu yake ina macho, huliona lango hata akiwa amegeukia nyuma.

Anakutana na Dante ambaye ni mzuri kwa mipira ya angani na ardhini, ni mzuri sana kwa kufanya ‘man to man marking”

Kagere

 kama Dante akipewa jukumu la kumuangalia Meddie basi kutakuwa na battle la aina yake. Dante atalazimika kutumia nguvu nyingi kumzuia Kagere, na kumnyima nafasi ya kushuti.

Kelvin Yondani, kama kawaida yake, kazi yake ni kusafisha mipira inayozagaa, lakini jukumu hili huenda likaingia mushkeri kutokana na uwepo wa Bocco ambaye hucheza kama mshambuliaji asiyetulia eneo moja, yeye hutafuta mipira inayozagaa hovyo na kuigeuza kuwa magoli.

Kazi hiyo ya Bocco inakinzana na majukumu ya Yondani na hapo ndipo vita huanzia. Bocco hana undava kama Yondani, mwenye silaha nyingi zikiwemo zile za kutumia nguvu nyingi bila sababu na kubwa ni silaha ya maneno na vitendo.

Wahambuliaji wa Simba wanaweza kutumia udhaifu huu beki za Yanga, kupata penati na hata kumzawadia mtu kadi nyekundu. Hakika itakuwa ni vita moto na si baridi kati ya safu hizi mbili za ushambuliaji na ulinzi.

  7.Ajib vs Aishi  Manula.

Mechi dhidi ya Al Ahly, uwanja wa taifa, Manula alikuwa vizuri zaidi. Alionyesha ni kwanini wanamuita “Tanzania One” . Manula amekuwa na kiwango kisichotulia kwa mechi kadhaa zilizopita, mashuti ya mbali yalikuwa changamoto kwake.

Jumamosi hii atakutana na miamba ya soka nchini, Young Africans chini ya nahodha Ibrahim Ajib, katika kiwango chake japo ni cha kusua sua.

Ajibu, wengine wanapenda kumuita mguu wa dhahabu, dhahabu hii ni kutokana na matumizi mazuri katika upigaji wa mipira ya kutenga(free kicks). Manula atakuwa na shughuli pevu kuzuia mipira ya Ajib kutikisa nyavu zake. Hadi sasa Ajibu ndiye anayeongoza kwa kutoa pasi nyingi za magoli (zaidi ya 11) nyingi ya pasi hizo ni mipira ya kutenga zikiwemo kona.

Aishi

Kama ilivyokawaida, mipira ya kona, mchezaji wa kwanza anatakiwa kuokoa ni Manula. Mipira yote ya “free kick” nayo ni jukumu la Manula kuiokoa.

Hili  ni battle binafsi, usilipimie kabisa, Manula atataka kutoa “clean sheet” itakayo msaidia kuwa golikipa bora mwisho wa msimu, huku Ajibu tangu awe nahodha amefunga goli moja pekee, naye atahitaji kujiongezea mtaji wa magoli hasa kwa kumtungua golikipa bora kama Manula.

             8. Heritier Makambo vs Sergie Paschal Wawa.

Hakuna ubishi kuwa tegemeo la Yanga katika nafasi ya ushambuliaji ni Makambo. Makambo ambaye tayari ametia kimiani magoli 11, na kuiweka timu yake kileleni mwa msimamo wa ligi kuu.

Makambo amekuwa ni mwiba kwa timu pinzani kwa kuitumia vizuri mipira ya vichwa na hata ya chini. Amekuwa na kasi na uwezo wa kutembea na mpira. Ni muziki akikutana  na Wawa, Wawa ambaye morali yake imeonekana kupanda baada ya kumpuliza Al Ahly.

Udhaifu wa Wawa ni uzito kwa mipira “one against one” kutakuwa na kazi kubwa kama tu Makambo atakuwa “sharp” anapolitazama goli la Simba.

Kazi ya Wawa itakuwa nyepesi kama atacheza pamoja na Juuko Mursheed ambaye hataki utani kabisa linapokuja suala la ulinzi. Juuko atakuwa msaada mkubwa sana katika kupunguza kasi ya Makambo na yeyote atakayecheza eneo la juu. Pia kama Zahera atakuja na mfumo wa 4-5-1 kazi itakuwa nyepesi kwa mabeki hao wa kati kuidhibiti safu ya ushambuliaji ya Yanga.

Je nani atamshinda mwezake katika “battle” hizi? Kila timu na kila mchezaji anahitaji kupata ,matokea katika mechi hii, Mashabiki wa Simba wanaamini kuwa ushindi katika mechi ya Yanga ni kuukaribia ubingwa, hata kwa Yanga nako mambo yapo hivyohivyo.

Battle hizi zitajidhihirisha endapo tu, Yanga itakuja na kikosi hiki; Kabwili, Gadiel, Yondani, Dante, Godfrey, Tshishimbi, Feisal, Ajibu, Ngasa, Matheo/Buswita na Makambo. Kwa upande wa Simba;Manula, Coulibaly, Wawa, Juuko, Tshabalala, Kotei, Mkude, Chama, Okwi,  Kagere na Bocco.

Wawa

Mabadiliko yoyote yanaweza kutokea lakini kutokana na “game plan” za makocha na mifumo, mpambano katika safu ya ulinzi utakuwa ni wakutosha na safu ya ushambuliaji ya timu pinzani, bila kusahau katika nafasi ya kiungo, ambayo ndiyo inayoonekana kuwa mwamuzi mkuu wa mechi hii kwa kutengeneza nafasi za magoli.

Tangu mwaka 1965, Simba na Yanga wamecheza mechi 101, Yanga akishinda michezo 36, sare 35 na kufungwa mechi 30. Simba akishinda michezo 30, akitoa sare mara 36 na kupoteza michezo 36. Yanga imejikusanyia alama  143 huku Simba ikijikusanyia pointi 125 katika michezo yote 101 waliyokutana, je Simba kupunguza “gap” la alama au Yanga kupanua gap hilo? tukutane taifa.


Sambaza....