Baada ya kushuhudia klabu ya soka ya Juventus ikitawazwa bingwa wa ligi kuu ya Italia kwa mara ya nane mfululizo mwishoni mwa Juma lililopita, inawezakana Barcelona nao wakatangazwa mabingwa wa ligi kuu Uhispania usiku huu.
Barcelona ambao usiku wa kuamkia leo wamefanikiwa kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Alaves wanasubiri kwa hamu kujua matokeo ya Atletico Madrid ambao wanacheza na Valencia usiku huu.
Ikiwa kama Atletico watafungwa na Valencia basi Barcelona ambao wapo kileleni kwa tofauti ya alama 12 watakuwa mabingwa kwa msimu mwingine wakiwa wamebakiza michezo minne kumaliza msimu.
Barcelona wapo kileleni kwa alama 80 na hata kama Atletico watafanikiwa kushinda michezo yote mitano waliosalia watafikisha alama 83 ambapo kama Barcelona watashinda mchezo wao unafuata basi watanyakuwa ubingwa kwani itatumika njia ya ‘Head to Head’ ikiwa Barcelona atashindwa kabisa kuongeza alama katika michezo itakayobakia.
Kwa mantiki hiyo hakuna namna yoyote ambayo itawazuia Barcelona kuchukua ubingwa wao wa 26 wakiwa nyuma ya Real Madrid ambao wao wamechukua taji hilo mara 33 toka ligi hiyo ilipoasisiwa mwanzoni mwa karne ya 20.
Katika mchezo wa jana mabao ya Barcelona yalifungwa na kinda mwenye umri wa miaka 21 Carles Alena kabla ya Luis Suarez kufunga bao la pili kwa njia ya penati baada ya VAR kuonesha kuwa mchezaji wa Alaves aliunawa mpira ndani ya 18.