Jua linachomoza ikiwa ni ishara ya mwanga kwenye maisha ya mwanadamu yoyote yule aliyepanga kwenye nyumba inayoitwa dunia.
Nyumba ambayo tunapita, nyumba ambayo imebeba watu wenye nia na malengo mbalimbali ili kufikia mafanikio.
Mafanikio hufikiwa pale panapokuwa na msukumo wa mtu mwenyewe kutaka kufanikiwa ndiyo maana kuna mtu aliwahi kusema “bora ya mwelekeo kuliko kasi”.
Unaweza ukakimbia sana tena kwa kasi kubwa zaidi ya kasi ya Usain Bolt lakini ƙkasi yako ikawa haina tija kama hauna mwelekeo.
Unaelekea wapi kipindi unapokimbia?, Unafuata nini?, kwanini utumie muda na akili kukimbia kwenye uelekeo uliouona ni sahihi?.
Hapa ndipo tunapotofautiana wengi sana, kuna wengine hukimbia ili waonekane wapo kwenye mbio lakini hukimbia bila malengo ( mwelekeo).
Haijalishi urefu au ufupi wa hatua unazopiga cha muhimu ni wewe kuhakikisha unapiga hatua za uhakika hata kama ni hatua fupi fupi. Uhakika wa hatua zako ndiyo utakufanya wewe ufike unapopatamani kila siku kufika.
Muda ndiyo jibu sahihi ya safari yako, ndiyo maana kuna muda Coastal Union iliwapa taa Abdi Banda na Juma Mahadhi, macho ya wengi yakawaona kutokana na nuru iliyotengenezwa na Coastal Union juu yao.
Simba haikusita mara mbili kuingiza mkono wake kwenye mfuko wa suruali kutoa pesa za usajili kwa ajili ya Abdi Banda na Yanga nao hawakutaka kuwa mabubu, walipaza sauti yao mpaka Tanga, sauti yenye ushawishi, ushawishi ambao ulimfanya Juma Mahadhi atoke Tanga na kuja kuishi Jangwani.
Kariakoo pakawa makazi yao mapya, makazi ambayo yanaaminika kama daraja la wengi kupitia kwenda sehemu yenye malisho bora zaidi.
Kila mtu alitegemea vipaji hivi vitafika mbali. Nafasi ya kucheza kwenye timu zenye ushawishi mkubwa nchini waliipata.
Kilichokuwa kimebaki ni kuona miguu yao wakiitumikisha kufika sehemu ambayo ni kubwa.
Hapa ndipo utofauti wa kukimbia kwa kasi na kukimbia ukiwa na mwelekeo ulipoanza kuonekana.
Kuna mwingine alionekana anakimbia kwa mwelekeo ndiyo maana mpaka sasa hivi hatupo naye kwenye ligi yetu hii ya kiswahili.
Kuna mwingine alionekana anakimbia kwa kasi sana bila kujua ni wapi anapokimbilia. Hata alipopewa kuwakabili TP Mazembe alionekana ana hasira sana , lakini hasira ile ilikuwa ya muda tu.
Muda wa kifurushi cha hasira chake kilipoisha ndipo hapo akarudi kwenye uhalisia wake. Uhalisia ambao umemfanya kila siku abaki sehemu ile ile aliyopo.
Hakuna jitihada madhubuti kwake yeye kupigana na kusogea mbele zaidi. Kila uchwao giza linaongezeka mbele yake, hana taa, hana kiberiti hata mawe ya kugonganisha ili apate mwanga aone uelekeo wa kukimbilia.
Kuna kipindi ukimwangalia usoni mwake unaona taswira inayozungumza kuwa anaonewa, hapana shaka uso wake unasema vitu vingi vilivyomo moyoni mwake, benchi la ufundi la Yanga linambania?
Huitaji mwaka mzima kuudhibitishia ulimwengu kuwa unaweza ukaleta mabadiliko yenye tija, Juma Mahadhi hupewa nafasi ya kucheza hata kama yeye anaona ni nafasi finyu lakini nafasi hiyo hiyo finyu anaweza kuitumia kutengeneza mwanga wa maisha yake ya soka.
Hatakiwi kufikiria dakika 90 ndizo zitakazomfanya aweze kuonesha kuwa anastahili namba katika kikosi cha Yanga.
Binafsi naamini kupitia katika kipaji cha Juma Mahadhi lakini kinachokosekana kwake ni yeye kushindwa kutofautisha kati ya kukimbia kwa kasi na kukimbia kwenye mwelekeo sahihi, mstari huu ndiyo uliowatenganisha yeye na Abdi Banda.
Natamani asome makala hii.
Yanga ipo katika michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika, kombe ambalo linatoa fursa nzuri ya wachezaji kujiuza vipaji vyao.
Ni muda sahihi kwa Juma Mahadhi kuacha kukimbia kwa kasi bila uelekeo, anatakiwa atazame uelekeo sahihi ili akimbie kwa malengo.
Dakika chache anazopewa ndani ya kikosi cha Yanga zisiwe dakika ambazo zinamdidimiza, asifikirie kabisa anaonewa na benchi la ufundi kupewa dakika chache kwenye mechi, ila anatakiwa ashukuru amepewa nafasi ya ƙkujiinua na kukimbia kwenye uelekeo sahihi.
Muda huu ni muda sahihi kwake yeye kuutumia kufika alipo Abdi Banda.
Muda unaruhusu, nafasi anayo cha muhimu ni ƴyeye kuona ukubwa na thamani ya kila sekunde anayopata uwanjani.