Sambaza....

Kabla sijakupeleka mbali, kwanza vuta taswira ya paka, kisha mkaribishe kocha wa Simba SC, Patrick Aussem katika medulla ya ubongo wako kisha anza kumtafsiri kwa kukumbuka kama ndiye aliyeirudisha historia iliyoadimika kusikika kwa wekundu wa msimbazi na nchi kwa ujumla baada ya miaka 15 kabla ya kufuzu raundi ya makundi klabu bingwa barani Africa.

Paka ni mnyama mdogo kwa muonekano, lakini ni miongoni mwa wanyama maarufu duniani haswa kwa sababu ya sifa zake na kuishi na binadamu, kiufupi paka ni rafiki wa binadamu. Lakini urafiki huo unaweza kuisha mara moja kama tu, utamuingilia kwenye anga zake.

Macho ya paka yana sifa ya kuona mbali hasa usiku kukiwa na giza. Binadamu kukiwa na giza yeye haoni lakini paka anaona. Hapohapo macho yake wanakuwa yanawaka wakati wa usiku, kisayansi hii ni kutokana na jicho la paka kuwa na safu ya tishu zijulikanazo kama “tapetum Lucidum”. Hivi utaniamini kama nikikwambia kuna makocha wa soka, ni kama paka? Achana na Guardiola wa Man City, hapa namzungumzia Aussem wa Simba.

Unaweza kushangaa, kikosi kile cha Simba kinafungwaje na Mbao, au kinatokaje sare na Wanapaluhengo, Lipuli FC, bila shaka ungemuuliza swali hili Aussem angekujibu kuwa kila mechi ina mahitaji yake na mbinu zake kiufundi.

Jicho la kocha ni la kitaalamu, linaona mbali, sehemu palipo na giza lenyewe ndio linaona vizuri kabisa. Muone Aussem alivyowachanganya wachambuzi na wadau wa soka nchini kwa kurudia kikosi kilekile kilichopoteza nchini Zambia kwa goli 2-1 dhidi ya Nkana licha katika mchezo huo kikosi hicho kilionesha udhaifu mkubwa katika kila idara kuanzia golikipa hadi washambuliaji.

Mabeki, Erasto Nyoni  na Paschal Wawa walishindwa kuelewana, Mohamed Hussein na Nicolus Gyan walikuwa uchochoro, wengi waliamini kuwa, Gyan angempisha Erasto na kuingia kwa Juuko Murshid kama ingizo jipya kwenye kikosi lakini Aussem ameamua kumrudisha Gyan katika nafasi ya ubeki.

KWANINI GYAN?

Nikisema Aussem ana macho ya paka, namaanisha hiki cha kumpanga Gyan kwenye mechi muhimu kama ile. Aussem alimpanga Gyan kwa sababu kuu mbili. Kwanza ni sababu ya kisaikolojia. Kisaikolojia Gyan alikuwa na faida kutumika kuliko mtu mwingine, Gyan ameaminiwa kwa mechi zote za klabu bingwa bila shaka ile thamani ya kuaminiwa na mwalimu  kumemjengea ari kubwa na mchezo na ndio maana hata alipoamua kumtoa, tayari alikwisha mpa alichotaka kwa kutoa pasi ya mwisho iliyozaa goli la  kuongoza la Meddie Kagere. Hapa ni dhahiri kuwa Aussem haku-bet kumpanga Gyan bali ni maono yake kisaikolojia yamemfanya ampange.

Pili, ni kutokana na asili ya Gyan mwenyewe. Kiasili Gyan ni mshambuliaji, na hata aliposajiliwa kutoka Ghana, alikuja kwa matumizi ya ushambuliaji lakini alibadilishwa na kuwa beki. Kumpanga mtu kama Gyan ni kuitaka timu ishambulie kupitia pembeni, na Gyan amelitekeleza jukumu hilo kwa zaidi ya asilimia 70 na kusaidia kupatikana kwa goli la pili katika dakika za nyongeza za kipindi cha kwanza. Aussem alilazimika kumpanga beki wa sampuli  ya Gyan kwa sababu timu ilikuwa nyuma kwa goli 2-1.

Haya turudi kwa paka.Mbali na kuwa macho yanayoona kwenye giza pia ana masikio yenye sifa nyingi. Sikio la paka lina misuli 32 inayomuwezesha kulizunguusha sikio lake hadi nyuzi 180 na kuipata sauti ya kitu hata kama kiko mbali. Paka ana uwezo wa kuitambua sauti ya kitu chochote na kuichuja sauti hiyo, ndio maana unaweza ukamuita paka akakusikia lakini asikufuate.

Wachambuzi wangapi wamemuandikia Aussem juu ya kikosi cha Simba, hasa udaifu wake katika maeneo ya mabeki, kiungo na washambuliaji? Je ni nani aliyepata nafasi ya kusikilizwa?. Wachambuzi wengi wa soka walikuwa wanaamini kuwa kuwaanzisha washambuliaji watatu yaani John Boko, Kagere na Emmanuel Okwi ni makosa kwakuwa wanaamini kuwa Simba ikiwa na mfumo huo huzidiwa eneo la kati hasa kile kiungo cha juu baada ya James Kotei na Jonas Mkude kuwa viungo wa chini hivyo akizidiwa Clatus Chama basi timu nzima itakuwa imezidiwa, na hii ilijidhihirisha katika mechi ya kwanza dhidi ya Nkana nchini Zambia.

AUSSEM ANAWAZAJE?

Aussem yeye anaamini kuwa, Okwi, Kagere na Boko wanastahili kucheza pale ndio maana katika mechi zote za kimataifa, mastraika wote watatu aliwaanzisha. Mara nyingi Okwi na Chama hucheza kama viungo wa juu, wakipishana uelekeo wa kutokea yaani mwingine hutokea kushoto na mwingine kulia, huku Kagere au Boko mmoja wao hukaa pale mbele ili kuwafanya mabeki wa timu pinzani washindwe kupandisha timu. Jukumu la kukaa pale mbele kama straika wa mwisho mara nyingi anayeliweza ni Kagere, Boko hushindwa kulitendea haki kwakuwa anatabia ya kuufuata mpira. Kagere alidhihirisha hiki ninachokisema katika mechi ya kwanza dhidi ya Nkana, ambapo alikwatuliwa kwenye boksi na kuizawadia Simba penati na kisha kupata goli la ugenini.

Sifa za paka haziishi, lakini mwisho kabisa Waswahili wana msemo wao maarufu unaomuhusu paka “Paka ana roho saba”, hii ni kutokana na imani kuwa, paka hafi kirahisi, hata umpige na mawe, ukidhani umemuua lakini ukirudi kesho humkuti.

Utajuaje kama Ausem ana roho ya paka?

Utamjua Aussem kwa dalili. Acha nikuonyeshe hizo dalili, nazo ziko tatu. Kwanza, kukaa kama kocha mkuu bila ya kuwa na msaidizi. Uwepo wa kocha msaidizi kuna faida zake hasa katika mgawanyo wa majukumu ambapo ingesaidia klabu kuwa na uwiano sawa kiutendaji, hakuna atayeelemewa na majukumu na kusababisha udhaifu katika klabu. Aussem anajaribu kuepusha migogoro ya kifalsafa ambayo ingejitokeza kati yake na kocha msaidizi hasa ukiwa na kocha msaidizi kama Masoud Juma ambaye mfumo wake wa 3-5-2 ulianza kuwanogea Simba, na hii ndio sababu ya kuachwa kwa Pierre Lechantre.

Pili, ni kufanya mabadiliko kulingana na uhitaji bila kujali anayemtoa ni nani. Una kumbuka mechi ya kwanza dhidi ya Nkana, kule Zambia? Alifanya mabadiliko kwa kumuingiza Shiza Kichuya na kumtoa Okwi, ambapo mchezaji huyo hakuonesha kufurahishwa na maamuzi ya kocha, lakini baadae Kichuya alitoa pasi iliyosababisha kuangushwa kwa Kagere na kupata goli la ugenini. Hivyo mabadiliko ya Aussem yalizaa matunda kuliko angemuacha Okwi uwanjani.

Tatu, ni kuiamini na kuishi na falsafa yake hata kama, falsafa hiyo inamuangusha. Mbinu aliyoitumia dhidi ya Mbababe ndio hiyo hiyo aliyotumia dhidi ya Nkana kwa mechi ya ugenini na nyumbani na ndio hiyo hiyo anayoitumia katika michezo ya ligi kuu Tanzania bara.

Tabia yake inanikumbusha  Milan ya Arrigo Sacchi na Fabio Capello ambayo ilipata mafanikio makubwa kutokana na makocha hao kushikilia falsafa zao kwa muda mrefu bila kuziacha hata kama kuna wakati zinawaangusha. Mfano matumizi ya mfumo wa 4-4-2 ndio mfumo uliyoiweka klabu hiyo kuwa maarufu miaka ya  80 na 90 baada ya kuisaidia klabu kubeba vikombe mbalimbali vikiwemo vya kimataifa na vya dunia kama “Uefa Super Cup” mwaka 1988 hadi mwaka 1995 lakini kumbuka pia, mfumo huo huo chini ya kocha yuleyule, Fabio Capello, Uingereza ilitolewa katika mashindano ya kombe la dunia mwaka 2010  na Ujerumani iliyokuwa ikitumia mfumo wa  4-2-3-1 lakini Capello hakuwahi kuikatia tamaa falsafa yake.

Kocha bora ni yule aliye tayari kufa na falsafa yake, yaani hayupo tayari kuisaliti kutokana na ushawishi wa watu ndani na hata nje ya klabu.

Simba imerudia kile ilichokifanya mwaka 2003 ikiwa ni miaka 15 tangu ilipofuzu hatua hii ya mtoano na kuingia makundi kwa goli la Marehemu Christopha Alex Masawe (Mungu amrehemu) dhidi ya Zamalek ya Misri. Simba sasa itarajie kukutana na timu kama Asec Memosas, Al Ahly, AS Vita, Saoura(Algeria), Club Africain, Al Nasri (Libya), Mamelod, Platinum,Constatine, Mazembe, Orlando Pirates, Lobi, Cotton, na Jarafu ambazo tayari zimeshafuzu. Hatua hii lazima iwe na mbinu na mikakati (approach) yake tofauti na hatua za mtoano.

Sambaza....