Klabu ya soka ya Arsenal Jumatatu hii, imetangaza kuingia mkataba na kampuni ya utengenezaji wa vifaa vya michezo ya nchini Ujerumani Adidas, mkataba ambao unatarajiwa kuanza Julai mwakani.
Adidas watachukua nafasi ya Puma ambao mkataba wao wa miaka mitano na klabu hiyo ya Kaskazini mwa London unafikia tamati mwishoni mwa msimu huu.
Vyombo vya habari nchini Uingereza vimeripoti kuwa mkataba kati ya Arsenal na Adidas umegharimu kiasi cha Dolla Milioni 391.7 ambayo ni sawa na Shilingi Bilioni 895.8 wenye muda wa miaka mitano hadi 2024.
Kwa mantiki hiyo Kila mwaka Adidas watalazimika kutoa kiasi cha Shilingi Bilioni 179, kiasi kitakachowafanya kuwa klabu ya tatu kwa vilabu vinavyoramba mkataba mnono wa vifaa vya michezo, wakiwa nyuma ya Barcelona ambao wanamkataba na Nike wenye thamani ya Shilingi Bilioni 417 na Manchester United wenye mkataba na Adidas wenye thamani ya Shilingi Bilioni 224 kwa mwaka.
Ikumbukwe kabla ya Arsenal kuwa na mkataba na Puma walikuwa wakivalishwa na Nike kwa miongo miwili, na mara ya mwisho Arsenal kuvalishwa na Adidas ilikuwa ni kati ya mwaka 1986 na mwaka 1994 walipotwaa mataji mawili ya ligi.
Taarifa zinasema kuwa baada ya puma kuachana na Arsenal watatangaza kuingia mkataba na Manchester City mkataba ambao utakuwa na thamani ya shilingi bilioni 149 kwa mwaka, mkataba ambao unaweza kuanza katika msimu wa 2019-20.