Kiungo mshambuliaji Hassan Dilunga na Beki wa pembeni Asante Kwasi wataukosa mchezo wa ligi dhidi ya Mbao FC utakaofanyika siku ya Alhamis kwenye uwanja CCM kirumba kutokana na kuwa na Majeraha.
Kocha mkuu wa Simba Patrick Aussems amesema wachezaji hao wanaungana na Mzamiru Yassin ambaye naye bado ana majeraha kuwa sehemu ya wachezaji ambao wataukosa mchezo huo pengine na ule dhidi ya Mwadui utakaopigwa mwishoni mwa Juma mjini Shinyanga.
“Tupo hapa Mwanza na wachezaji 21, kujiandaa na michezo miwili ya ligi, mchezo wa Alhamis na ule wa Jumapili, bado tunachezaji ambao wana majeraha, kuna Yassin, Dilunga na Asante kwa hiyo wachezaji hao watatu hawatakuwa sehemu ya michezo hiyo,” Aussems amesema.
Aussems amesema licha ya kuwakosa wachezaji hao lakini bado ana hazina kubwa ya wachezaji aliosafiri nao na anachoamini anaweza kupata ushindi, kwani huu utakuwa mchezo wa pili nje ya Dar es Salaam.
“Tumecheza michezo miwili nyumbani na tulishinda, lakini mechi iliyopita tumecheza ugenini na tulicheza na mpinzani imara kidogo ambaye alikuwa anajilinda sana na tulitoka sare, na nafikiri hii ndiyo hali ambayo tutakutana nayo katika kila mchezo, kwa hiyo tunahitaji kuwa makini zaidi, na tupo tayari kwa hilo,” Aussems amesema.
Mpaka sasa Simba imeshacheza michezo mitatu na tofauti na matarajio ya wengi imefanikiwa kushinda michezo miwili ya Nyumbani na kutoka sare mchezo mmoja wa ugenini dhidi ya Ndanda, matokeo ambayo yanawafanya kufikisha alama saba.
Wakiwa katika mikoa ya Kanda ya Ziwa Simba watacheza michezo miwili dhidi ya Mbao siku ya Alhamis na baadae watacheza na Mwadui kwenye uwanja wa CCM Kambarage siku ya Jumapili kabla ya kurejea jijini Dar es Salaam kucheza na Biashara United.