Shirikisho la soka nchini Nigeria (NFF) limetangaza kumfungia kocha Salisu Yusuf kwa muda wa mwaka mmoja, sambamba na kumtoza faini ya dola za kimarekani 5000.
NFF imefikia hatua ya kumuadhibu Yusuf mwenye umri wa miaka 56, baada ya kujiridhishwa alihusika na sakata la kupokea rushwa.
Yusuf alionekana katika picha za video, akipokea fedha kinyume na taratibu kutoka kwa mtu aliejitambulisha ni wakala wa soka, ili afanikishe utauzi wa wachezaji wawili kupitia michuano ya continental championship.
Kamati ya maadili ya NFF imetoa taarifa za kufungiwa kwa kocha huyo, na kuwataka wadau wote wa soka barani Afrika kutoshirikiana na Yusuf katika shughuli zozote zinazohusu mchezo huo.
Taarifa ya kamati imeeleza kuwa “Yusuf alipokea fedha kutoka kwa wakala aliejitambulisha kuhusika na wachezaji wa Tigers (Osas Okoro na Rabiu Ali) ili awaite kwenye kikosini cha Nigeria kilichoshiriki michuano ya Mataifa Bingwa Ya Afrika CHAN mwaka 2018 nchini Morocco.”
Yusuf alikua msaidizi wa kocha Gernot Rohr wakati wa fainali za kombe la dunia nchini Russia, na alikua kocha mkuu wa kikosi kilichoshiriki fainali za Mataifa Bingwa Ya Afrika (CHAN) nchini Morocco