Kiongozi wa klabu ya Friends Rangers inayoshiriki ligi daraja la kwanza Tanzania Bara, Henry Mzozo amesema wanatarajia kuweka kambi wilayani Lushoto mkoani Tanga kabla ya mchezo wao wa kwanza ligi hiyo.
Mzozo amesema kambi hiyo inatarajia kuanza Septemba 10 na wakiwa huko watacheza mechi kadhaa za kirafiki kabla ya kuanza kwa ligi ambayo mpaka sasa bado ratiba yake haijatoka licha ya makundi kutangazwa.
“Tutakaa Lushoto kwenye kambi maalumu kuanzia Septemba 10 hadi 20, tumeambiwa ligi inaweza kuanza mwishoni mwa mwezi huu au mwanzoni mwa mwezi wa kumi, hivyo tukitoka Lushoto tunaamini zile siku 10 zitatutosha kumalizia maandalizi ya ligi,” amesema.
Friends Rangers wapo kundi A la ligi daraja la kwanza pamoja na timu za Ashanti United, Dar City FC, Kiluvya United, Majimaji, Mawenzi FC, Mbeya Kwanza, Mlale FC, Mufindi United, Namungo FC, Njombe Mji na Reha FC ya Dar es Salaam.