Sambaza....

1: Golikipa.

Moja ya eneo ambalo ni muhimu kwenye timu ni eneo la golikipa, siku zote golikipa ndiye mshambuliaji wa kwanza na ndiye mtu ambaye anaifanya timu iwe hai muda mwingi mwa mchezo. Lakini hii imekuwa tofauti sana kwa Youthe Rostand. Amekuwa golikipa ambaye ana makosa mengi akiwa langoni. Mfano siyo mzuri kucheza mipira ya juu na krosi pamoja na kwamba ni mrefu. Kabwili anaonekana ni mdogo kiumri lakini mikono yake imekomaa na maamuzi yake yamekomaa kuzidi maamuzi ya Youthe Rostand.

2: Beki wa Kati ambaye ni kiongozi.

Moja ya makosa ambayo Yanga walikuwa wanafanya katika mechi dhidi ya USM Alger ambayo walifungwa goli 4-0 ni wao kuwa na safu ya ulinzi iliyokuwa inafanya makosa kwenye “marking” pia ilikuwa inakosa kiongozi wa kuwaongoza katika safu yao ya ƴulinzi. Kukosekana kwa Kelvin Yondani kulionekana ni tatizo kubwa sana kwa Yanga. Leo hii wanamwihitaji Kelvin Yondan kwa kiasi kikubwa kama kiongozi mzuri, kiongozi ambaye atahakikisha Yanga kutokuwa na makosa binafsi katika eneo la nyuma.

Pia kwenye mechi ya USM Alger, Yanga walikuwa wanakosa mtu wa kuanzisha mashambulizi. Mara nyingi Kelvin Yondan licha ya kwamba amekuwa ni beki mahiri kwenye kukaba lakini anaweza kuanzisha mashambulizi kwenye timu.

3: Eneo la kiungo cha Kati.

Kwenye mechi ya Yanga dhidi ya USM Alger, Yanga ilionekana safu yake ya ushambuliaji ikiwa imetengwa kwa kiasi kikubwa kwa sababu hakukuwepo na kiungo ambaye alikuwa anaiunganisha safu ya kiungo ya Yanga na safu ya ushambuliaji ya Yanga. Sasa leo Yanga wafanye nini? Kutokuwepo kwa Papy “Kabamba” Tshishimbi na Kamusoko kutokuwepo kwenye kiwango kizuri tangu atoke kwenye majeraha kunaweza kuwa sababu ya Yanga kuwatumia vijana ambao wanaweza kuleta faida isiyo tarajiwa. Mfano, Edward Makka pamoja na umri wake kuwa mdogo lakini amekuwa na uwezo wa kuiunganisha timu. Hivo akicheza pamoja na Raphael Daud wanauwezo mkubwa wa kuiunganisha timu na safu ya ushambuliaji kuonekana kutotengwa.

4: Safu ya ushambuliaji.

Obrey Chirwa hakuwepo katika mechi dhidi ya USM Alger na ndiye mshambuliaji ambaye amekuwa nguzo muhimu katika kikosi cha Yanga msimu huu. Kuwepo kwake kutakuwepo na faida kwa Yanga.

Sasa kuwepo kwake pekee kunatosha?

Kuwepo kwa Obrey Chirwa bila Yanga kuhakikisha inatumia vizuri nafasi wanazozipata haitokuwa na faida yoyote. Yanga wanatakiwa watumie vizuri nafasi wanazopata ili kuhakikisha wanatumia vizuri uwanja wa nyumbani.

5: Kutofikiria hali inayotokea kwa sasa ndani ya klabu.

Hakuna cha kuficha kuwa klabu kwa sasa inapitia ukata mkubwa sana. Hivo hali hii wanatakiwa kuiacha nje ya uwanja kipindi ambacho wanaingia uwanjani na kupigana kwa ajili ya timu na maisha yao binafsi

Sambaza....