Kila mtu anamuonea huruma na kuna wakati mwingine huruma hizi zinaenda sambamba na sifa nyingi kuhusu kipaji chake.
Golikipa aliyedumu kwa muda mrefu tena kwenye kiwango chake bila kutetereka, miaka 40 inasomeka kwenye paji lake la uso lakini anadaka mipira ya mashuti ya vijana wa miaka (20-29)
Kuna wakati mwingine mikono yake imekuwa imara zaidi ya mikono ya makipa wenye umri mdogo. Mikono yake imekomaa ipasavyo na imedumu ipasavyo langoni
Hapana shaka mikono yake inastahiri kushika kila aina ya taji aliloshiriki kulipigania akiwa langoni.
Ubingwa mara nane wa Seria A ni kitu ambacho alistahili katika maisha yake na inawezekana wakati anakutana na Zinedine Zidane katika fainali ya kombe la dunia 2006 ilikuwa ni siku kubwa ya furaha kwake kwa sababu mikono yake ilinyanyua kombe la dunia.
Kombe lenye heshima kubwa dunia, kombe ambalo kila mchezaji anatamani kulichukua lakini bahati mbaya siyo kila mchezaji hufanikiwa kulishika kombe hili.
Kuna mengi sana ya kujivunia kwenye mpira, unaweza ukajivunia kubeba kombe la dunia mwenzako akakuuliza una medali ya mshindi wa kwanza ya kombe la ligi ya mabingwa barani ulaya?
Kombe ambalo lina hadhi kubwa kwenye ngazi ya klabu, unaweza ukafanikiwa kwenye timu ya taifa na ukabeba kombe lenye hadhi kubwa ngazi ya timu ya timu ya taifa, lakini ukashindwa kufikia mafanikio ya kubeba kombe lenye hadhi kubwa katika ngazi ya klabu.
Ndipo hapo huzuni lazima ikukamate tena unapogundua mchezaji nyota anamaliza maisha yake ya mpira wa miguu bila kubeba kombe la klabu bingwa barani ulaya.
Dunia ilimhurumia Ronaldo De Lima, ikaja kumuongelea kwa huzuni Zlatan Ibrahimovich leo hii inamuaga kwa huruma Gigi Buffon
Kipa ambaye hakuwahi kupata kadi nyekundu katika michuano ya klabu bingwa barani ulaya katika mechi 116 lakini mechi ya 117 Michel Oliver akamuonesha kadi nyekundu
Kadi ambayo ilikuwa na maana kubwa sana katika kuzima ndoto za Gigi Buffon, kadi ambayo ilikuwa na tafasri moja tu ni ngumu kwako kushinda kombe la klabu bingwa barani ulaya ukiwa kama mchezaji
Inawezekana ikawa mechi yake ya mwisho katika michuano hii ya klabu bingwa barani ulaya baada ya kufika fainali kwa mara mbili mfululizo bila kufanikiwa kushinda kombe
Anaondoka katika uwanja wa Santiago Bernabeu akiwa ameinamisha kichwa huku swali kubwa linalo muumiza ni lini atashinda kombe la klabu bingwa barani ulaya?
Moyo wake unatamani sana, mashabiki wengi wa mpira wanataka sana ashinde lakini muda haumruhusu tena yeye kushinda akiwa kama mchezaji
Kuna njia ambayo anatakiwa kuifikiria wakati huu anapojiuliza maswali hayo. Siyo muda sahihi kwake kuruhusu kuhurumiwa tena
Wakati huu anatakiwa atumie mlango wa pili, mlango ambao wengi wamefanikiwa baada ya kuingia huko.
Jana Zinedine Zidane alikuwa kwenye benchi la RealMadrid, timu ambayo aliitumikia kama mchezaji. Gigi Buffon anatakiwa akae chumbani kwake huku akiwa na picha ya Zinedine Zidane
Picha ambayo itamsaidia kukumbuka matukio ya nyuma ambayo yaliwahi kutokea kati yake na Zinedine Zidane.
Asilisahau tukio la mwaka 2006 tukio ambalo lilimwezesha kubeba kombe la dunia mbele ya Zinedine Zidane wote wakiwa wachezaji
Leo hii Zinedine Zidane ni kocha, tena kocha mwenye mafanikio makubwa, mshindi wa kombe la ligi ya mabingwa barani ulaya mara mbili mfululizo
Mafanikio haya yamtamanishe Gigi Buffon na kumfanya aone bado ana nafasi kubwa ya kubeba kombe la ligi ya mabingwa barani ulaya.
Muda haujamwaacha, nafasi bado anayo, ameshindwa kubeba kombe kama mchezaji lakini ana nafasi kubwa ya kubeba kama kocha.
Miaka 40 kwake ni mingi, ni wakati mzuri kwake kuvua gloves na kuvaa suti, ni wakati mzuri kwake yeye kusimama kwenye mstari wa makocha, siyo muda kwake yeye kusimama tena mbele ya milingoti mitatu
Amefanya kazi na makocha wengi wenye uwezo mkubwa wa kufundisha mpira, amekuwa nahodha kwa kipindi kirefu akiwaongoza wachezaji wenzake ndani ya uwanja, ni wakati mzuri kwake yeye kukaa kwenye benchi la ufundi na kuwaongoza wachezaji wa timu yake kubeba kombe la ligi ya mabingwa barani ƴulaya ili kutimiza furaha yake