KELELE za Donald Ngoma zimekuwa nyingi mitaa ya Jangwani. Dakika moja mwanachama huyu anazungumza hivi, dakika nyingine mwanachama yule anazungumza vile. Ngoma ndio ajenda kuu kwenye mazungumzo ya Yanga wakati huu.
Kalamu yangu inayomalizia saa chache huku fungate nayo imeshitushwa na Ngoma. Mjadala wake umetikisa hadi makundi ya WhatsApp niliyoko. Huko nako Ngoma ameteka comments nyingi za wachangiaji.
Baadhi ya rafiki zangu wa Yanga wameniambia Ngoma ni mtoro. Rafiki wa Ngoma wanasema Yanga haijamlipa Ngoma mshahara wake wa miezi kadhaa ndiyo maana Ngoma ameamua kujiweka kando na timu. Nani mkweli hapa?
Ninachokiamini kelele zote hizi tunazozisikia kuhusu Yanga na mchezaji wao, zinatokana na Yanga na sio Ngoma kama wengi wanavyodhani. Naamini hivi na siamini vingine. Nitakuja kuamini vingine siku ambayo Mkwasa ataamua kutoka hadharani na kuzungumza ukweli.
Mchezaji anayelipwa kila aina ya stahiki zake kwa wakati ni ngumu mtu huyu akadengua na kuamua kuondoka klabuni bila kuaga. Shida kubwa iliyoko robo tatu ya macho ya manazi wa Yanga yanaishia kwenye kingo nne za Tv. Ni kikundi cha watu wachache kinachofahamu jinsi Ngoma anavyoishi nje ya uwanja ambako hakuna kamera za Azam Tv wala mwandishi.
Kiburi hiki cha Ngoma kina kitu nyuma yake. Kuna kitu anachokitegemea ndiyo maana haoni shida kulala zake Harare kwenye hoteli moja ya kifahari na chai kuja kuinywa Dar es Salaam kwenye mgahawa wa Chief Pride.
Okwi ni moja ya mchezaji mahiri kama Ngoma. Hivi sasa ametulia Simba kutokana na watu wa Simba kuishi nae kwenye njia za ukweli. Siku ukiona Okwi amebeba begi lake na kuelekea Kampala, huku nyuma Simba ina mechi, fahamu kuna kitu hakikwenda sawa.
Ngoma juu ya kuonekana kama ana matatizo, tufahamu hana kazi nyingine zaidi ya mpira. Anapendwa kutokana na mpira, anatembelea magari ya kifahari kwa ajili ya mpira, analipwa pesa nyingi kwa ajili ya mpira. Mtu huyu anawezaje kuubeza mpira kirahisi? Ina maana sisi tunaipenda kazi yake hadi kumhurumia kuliko yeye? Kuna kitu Yanga hakiko sawa. Mkwasa aje hadharani tu.
Uliwahi kujiuliza kwanini kesi zote ambazo Okwi amewahi kuzipata akiwa Yanga, Simba, mara zote ameshinda yeye? Kabla ya kumlaumu Ngoma na kumuona msaliti aliyekosa adabu tunapaswa kutuliza fahamu zetu kwenye kulizungumza suala lake pole pole tutamuelewa nini anachomaanisha.
Inawezekana Kamusoko, Chirwa, Tambwe wakawa na hali kama aliyonayo Ngoma, lakini alichokifanya Ngoma ni kusema na moyo wake. Ni Ngoma na nafsi yake ndiye anafahamu nini kaja kufanya Tanzania, sisi tunaotoka povu juu ya masuala yake, tunajua karatasi zake za mikataba zinasemaje?
Ningekuwa na hofu kama Ngoma angekuwa Mtanzania. Tukiri kitu hapa. Mchezaji wa Kitanzania unaweza kumtimizia kila kitu chake bado akabeba begi na kurudi nyumbani kwao. Lakini kitendo cha Ngoma kuwa Mzimbabwe, naamini huyu anajua anachokifanya. Hajakurupuka hata kidogo.
Shida nyingine inayosababisha yote haya iko kwa baba yangu Mkwasa ambaye ni Katibu Mkuu wa klabu. Katibu Mkuu ndiyo Mtendaji wa kila siku wa shughuli za klabu. Mkwasa nae anasema hajatoa kibali cha Ngoma na kuongeza kuwa akirudi wanamkata mshahara. Jamani hapa mnamuelewa Mkwasa?
Kama Katibu Mkuu hapa tulitaraji kupata ukweli wa sakata hili, ili kila mmoja afahamu kilichosababisha Ngoma aondoke kwao, wakati anafahamu Yanga ina michezo inayomuhitaji. Narudia tena. Ni ngumu Ngoma kuondoka kirahisi, kukiwa hakuna matatizo.
Kama msumbufu inakuwaje wakati ule aliamua kutulia na kufanya kazi iliyomvutia kila mmoja, hivi sasa aonekane kama kinyesi?
Kuna kitu hakiko sawa. Muda huu ambao Yanga haina Mwenyekiti na Makamu wake akiwa beazy na shughuli za Bodi ya Ligi (TPLB), Mkwasa anapaswa kujitokeza na kuuzungumza ukweli. Hakuna namna.