Sambaza....

Nyuso zetu zimejaa furaha, furaha ya muda mfupi. Furaha ambayo imetusahaulisha kila tatizo lililopo katika familia yetu.
Familia yetu ina matatizo mengi sana, matatizo ambayo hayawezi kuondolewa na furaha ya siku moja

Tunajaribu kujificha nyuma ya shina la mchicha tukiiamini kuwa hatutoonekana, tunakosea sana kujaribu kujifuta machozi kwa leso ya mchanga.
Matatizo yetu hayawezi kusahaulika kwa ushindi dhidi ya DR Congo, sawa ni timu bora kuzidi sisi, inawachezaji wengi wanaocheza katika ligi za ulaya na kizuri zaidi inashika nafasi ya tatu kwenye ubora wa CAF.

Tumempiga kofi mbabe, hii haiaminishi tumeshafikia hatua ya kupigana na kila mbabe. Tusicheke na kufurahia sana mpaka tukasahau kumtengeneza mtoto atakayekuwa shujaa wa Taifa letu.

Mtoto ambaye atakuwa na malezi mazuri kuanzia chini mpaka atakapokua mkubwa tayari kwa kukipigana.

Mtoto huyu haji hivi hivi, ila kuna njia ambazo zinatakiwa kutengenezwa ili yeye apite mpaka awe mbabe kati ya wababe waliopo Afrika na duniani kwa ujumla

Turudi kwenye azimio la Bagamoyo, ambalo sisi wenyewe tulioona linafaa kwa sababu lilikuwa na mikakati ambayo ingetusaidia sana katika mpira wetu.

Miaka kumi na moja (11) tangu azimio hili lifikiwe lakini hatujafanikiwa kutekeleza hata robo ya vitu ambavyo tuliazimia katika azimio la Bagamoyo la mwaka 2007

Nilifurahia sana niliposoma kurasa iliyokuwa imeandikwa kuziagiza timu zote za ligi kuu kuwa na timu za vijana zilizo na umri wa chini ya miaka 14, 17 na 20.

Nilioona picha kubwa sana katika maendeleo yetu ya mpira kwa sababu mkondo huu wa kuwa na timu za vijana ulikuwa mkondo ambao ungepitisha maji ya vipaji vya soka kwa muda mrefu.

Nilijua ni wakati mzuri kwa TFF kuwa na ligi imara na iliyopangiliwa vizuri ili kuwapa nafasi vijana hawa kushindana. Matumaini yaliongezeka kwa kiasi kikubwa moyoni mwangu.

Nilijua kabisa mwanzo ungekuwa mgumu sana kwa sababu ya gharama za uendeshaji wa ligi kama hizi , lakini kuna kitu kilikuja kunifariji moyoni mwangu, kama TFF waliazimia mpango huu na wakauona mpango huu una manufaa makubwa basi watasimama kwenye kila hali mpaka pale mambo yatakapokuwa mazuri.

Hakuna mfanyabiashara asiyependa kuwekeza sehemu ambayo anaona ina manufaa makubwa kwenye biashara yake. Nilitegemea TFF wangetengeneza mazingira ya kuziuza ligi ya vijana hata kama ingechukua muda wa miaka mitano bila kupata mtu wa kuzinunua lakini kuna siku wangefanikiwa, mipango ya muda mrefu ya kibiashara ilihitajika kufikia hatua hii.

Hatua ambayo isingekamilika kama vilabu visingekuwa na timu hizi za vijana, timu ambazo zingetunzwa na kulelewa katika misingi mizuri ya mpira, misingi ambayo ingetuwezesha tupate wachezaji waliotoka katika mkondo mzuri.

Hatukufanya hivo, tukalipuuzia azimio la Bagamoyo ambalo liliwekwa na Leodigar Tenga. Kila kiongozi aliyekuja baada ya Tenga aliendelea kulipuuzia azimio hili.

Tumekuwa na viongozi ambao wanaamini katika wao, hawaamini katika mipango endelevu imara. Ni ngumu kumuona kiongozi akifanya kitu endelevu ambacho kilianzishwa na mtangulizi wake.

Miaka ilikimbia FIFA wakatuletea Club Licence , kitu ambacho kinaendana sana na Azimio la Bagamoyo.

Vitu vilivyokuwepo kwenye azimio la Bagamoyo ndivyo hivo vilivypkuwepo kwenye Club Licence. Vilabu vilitakiwa kuwa na timu za vijana, viwanja vya uhakika vya mazoezi na uwanja wa kuchezea, vifaa vya michezo kama jezi na Gym.

Lakini tulipuuzia, inawezekana ni ngumu kwetu sisi kumiliki Gym kutokana na uchumi wetu, lakini siyo ngumu kwetu sisi kufanya biashara na wamiliki wa Gym ili pande zote zinufaike, timu inufaike na mwenye GYM anufaike kwa kutangaziwa biashara yake.

Akili ya kibiashara haipo ndani ya viongozi wetu ndiyo maana kila kitu tunakiona ni kigumu kukitimiza kwa kiwango bora.

Wakati tukifurahia ushindi dhidi ya DR Congo tusisahau kuwa mpira wetu uko gizani tunahitaji taa ya kuliondoa giza hili na taa pekee ni kurudi katika misingi ya kisasa ya mpira, misingi ambayo itatusaidia kuzalisha wachezaji imara watakayoisaidia timu yetu ya Taifa

Sambaza....