Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa stars jioni ya jana imeibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya timu ya taifa ya Jamhuri ya kidemoklasia ya Kongo, katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki uliopigwa kunako uwanja wa taifa jijini Dar es salaam
Mchezo huo wa kalenda ya FIFA, ulishudiwa dakika 45, za kipindi cha kwanza timu zote zikishambuliana kwa zamu huku wageni wakionekana kutawala kwa kiasi fulani
Stars inayonolewa na Kocha Mzalendo, Salum Mayanga, iliandika bao lake la kwanza kunako dakika ya 75, kupitia kwa nahodha wake anayekipiga kunako klabu ya KRC Genk ya Ubeligiji Mbwana Samatta, akimalizia kazi nzuri ya winga Shiza Kichuya
Shiza Kichuya aliwainua tena vitini Watanzania kunako dakika ya 85, baada ya kuipatia Stars bao la pili kwa shuti kali nje kidogo ya eneo la hatari, baada ya kupokea pasi nzuri ya Mbwana Samatta
Mpaka mwamuzi Heri Sasi anapuliza kipyenga cha mwisho, kuashiria kukamilika kwa dakika 90, za mchezo Stars 2-0 Kongo
Stars iliingia katika mchezo wa leo, ikitoka kufungwa mabao 4-1 na Algeria Machi 22, katika mchezo mwingine wa kimataifa wa kirafiki wa kalenda ya FIFA
Kikosi cha Tanzania kilikuwa Aishi Manura, Shomali Kapombe, Gadiel Michael, Abdi Banda, Kelvin Yondan, Himid Mao/ Mudathir Yahya dk73, Mohammed Issa “Banka”/ Ibrahim Ajib dk60, Erasto Edward Nyoni, Mbwana Ally Samatta, Simon Msuva/ Yahya Zayed dk89, na Shiza Kichuya/ Rashid Mandawa dk88
DRC Ley Matampi, Issam Mpeko, Grody Ngoda, Yannick Bangala, Wilfred Moke, Aaron Tshibola/ Lema Mabibi dk47, Chancel Mbemba, Mubele Ndombe/ Junior Kabananga dk54, Needkens Kebano, Bennick Afobe/ Assombalanga Britt dk64 na Yannick Bolasie