Goli la mkono wa Mungu na goli bora la karne yalitokea katika mechi moja katika michuano ya kombe la dunia la mwaka 1986
Hapana shaka ilikuwa mechi ambayo ni ngumu k usahaurika virahisi kwenye kichwa cha Diego Maradona, hata kwetu sisi alituachia kumbukumbu ambayo ni ngumu kuisahau.
Hii ni baada ya miaka minne kupita baada ya vita kati ya England na Argentina iliyobatizwa kwa jina la “Falklands war”, vita nyingine ikatokea katika ardhi ya Mexico katika hatua ya robo fainali ya kombe la dunia la mwaka 1986.
Vita ambayo ilizalisha magoli mawili yaliyobaki kwenye kumbukumbu za wapenda soka, historia ilianza kuandikwa katika dakika ya 51 pale Diego Maradona alipofunga goli la mkono lililobatizwa kwa jina la “Hand of God”, zikapita dakika nne baadaye Diego Maradona akafunga goli la Karne ambapo alichukua mpira katikati ya uwanja na kukimbia nao huku akiwapiga chenga wachezaji sita kwa wakati tofauti, aibu ilianzia kwa Beardsley, akaipokea Reid ambayo akaona ampe Butcher aliyepokezana na Renewark ambaye alimwachia tena Beardsley ambaye alishindwa kumlinda golikipa Peter Shilton na kumfanya Diego Maradona kufunga goli la Karne.
Inawezekana England wanahistoria kubwa sana na ardhi ya Mexico, kabla ya mwaka 1986 , Mexico waliwahi kuandaa michuano ya kombe la dunia la mwaka 1970 . Michuano ambayo iliwezesha mboni za macho ya watu wengi kushuhudia mechi iliyokuwa na ushindani mkubwa sana. Historia inasema Mechi ya England na Brazil huwa ni mechi yenye ushindani mkubwa sana uwanjani, ushindani ambao hufanya mechi hii kuwa bora.
Ndiyo maana historia iliandikwa mwaka 1970 ambapo vitabu vya historia viliruhusu kurasa zake ziandike mchomo wa karne (save of the Century) uliotolewa na golikipa wa England Gordon Banks alipookoa kichwa cha Pele, kichwa ambacho kilionekana kabisa kinaenda golini lakini uajabu tulishuhudia mpira ukiokolewa na Gordon Banks, kila midomo ya walioshuhudia ilibaki wazi ikiwa haiamini kilichotokea , historia ikaandikwa na vitabu vitaendelea kumkumbuka Gordon Banks kama ambavyo vinavyomkumbuka Roger Milla na Cameroon yake ya mwaka 1990.
Argentina waliingia kama mabingwa watetezi kwenye michuano hii, watu wengi walikuwa na matumaini makubwa kwa timu hii kufanya vizuri lakini walishangaa ikifungwa na Cameroon ambayo ilikuwa haipewi nafasi kubwa sana na cha ajabu iliifunga Argentina ikiwa na wachezaji tisa (9) ndani ya uwanja
Nafasi ya kufanya vizuri kwetu sisi Waafrica huwa hatupewi sana, wenzetu huwa wanaamini sana kuwa wao ni bora na wanauwezo wa kufanya vizuri sana na ikitokea wamefanya vibaya majuto na kilio huwa ndani yao.
Ndiyo maana ni rahisi sana kumshuhudia mwanasoka wa ulaya akilia kilio kichungu na kizito kipindi timu yake inapokuwa inafanya vibaya.
Unamkumbuka Paul Gazza? Mchezaji ambaye tangu anakuwa aliamini kabisa yeye atakuwa mchezaji atakayechukua medali ya kombe la dunia ya mshindi wa kwanza?
Akiwa na miaka 25 alifanikiwa kuiwakilisha timu yake ya taifa ya England katika michuano ya kombe la dunia 1990 kule Italy.
Mechi ya nusu fainali dhidi ya Germany, machozi yalianza kumtoka alipopewa kadi ya njano, kadi ambayo ilimtoa mchezoni. Aliamini kadi ile ilikuwa na maana ya kwamba huo ndiyo mwisho wake. Aliumia sana akawa anaona ndoto zake za kuchukua ƙkombe la dunia zinafikia ukingoni, kilio kilizidi pale timu yake ya taifa ilipofungwa kwa mikwaju ya Penalti ikawa mwisho wa England na ndoto ya Paul Gazza.
Machozi yakabaki kwenye mashavu yake kama ambavyo mashavu ya Wafaransa wengi yaliyobaki yamelowana kwa machozi mwaka 2002 baada ya timu yake kushuhudia ikitoka kwenye hatua ya makundi.
Timu ambayo ilikuwa na wachezaji wengi nyota, na walikuwa mabingwa watetezi wa kombe la dunia pia wakiwa mabingwa wa kombe la Euro lakini waliaga mapema michuano hii tena kwa kufungwa na timu ambazo zilionekana timu za kawaida kama Senegal.
Na ndiyo michuano ambayo Senegal walifika robo fainali ya kombe la dunia na kuwa timu ya kwanza kufika hatua hii ya robo fainali. Mwaka 2010 Afrika tuliandaa michuano ya kombe la dunia, tukaamini ni nafasi nzuri kwetu sisi kuvunja rekodi ya Senegal, lakini Luiz Suarez alitukatili baada ya kudaka mpira uliokuwa unaelekea wavuni tukaishia hatua ya robo fainali.
Suarez akawa shujaa wao na akageuka kuwa adui wetu, chuki zikawa kubwa dhidi yake ndiyo maana hata alipopewa adhabu baada ya kumuuma begani Giorgio Chiellin katika kombe la dunia la mwaka 2014 nchini Brazil ilikuwa furaha kwetu sana.
Na hii ilikuwa mara ya pili kushuhudia wachezaji wa Italy wakifanyiwa vitendo vya ajabu katika michuano ya kombe la dunia baada ya kumshuhudia Zinedine Zidane akimpiga kichwa Matterazi katika kombe la dunia la mwaka 2006.