Sambaza....

Ni sehemu ndogo tu iliyopo Dar-es-Salaam, lakini ni sehemu ambayo ina umuhimu mkubwa sana hapa nchini, hapana shaka TRA hujivunia eneo hili. Hata wafanyabiashara hulitukuza eneo hili, utajiri wao ulianzia hapa na kukua hapa mpaka mitaani wakawa na heshima.

Hapana shaka ndilo eneo ambalo huwezi kuwa mchezaji wa mpira wa miguu bila kukanyaga, wengi wa wachezaji wetu wanaota kukanyaga eneo hili.

Ni mchezaji gani atafikiria mara mbili mkataba wa Mbao FC na kuuacha mkataba unaotoka kariakoo?

Ni shabiki gani wa mpira wa miguu hapa Tanzania asiyependa kushuhudia timu za kariakoo zikija mkoani mwake? , hugeuka siku ya historia na sikukuu kwa pamoja siku timu hizi mbili kutoka Kariakoo zinapofika kucheza mechi mkoa fulani

Tiketi huuzwa kwa wingi tofauti na mechi nyingine isiyohusisha timu moja wapo ya Kariakoo, wamachinga hutumia nafasi hiyo kuwaibia Yanga na Simba kuuza jezi ambazo bila ruhusa.

Pamoja na kwamba jezi zinazouzwa siyo jezi halali kutoka ndani ya vilabu hivi viwili vya kariakoo lakini mashabiki hununua kwa kiasi kikubwa.

Kipimo cha mapenzi ya mashabiki hawa kwa vilabu hivi viwili ni kikubwa mno, ndiyo maana hata mechi ya Simba na Yanga huwa ni sikukuu kubwa sana hapa nchini.

Barabara hupambwa kwa magari yenye bendera za hizi timu, vijiwe vingi vya kahawa hupeperusha bendera za hawa mahasimu wawili.

Image result for rAPHAEL DAUD

Biashara nyingi hufungwa mapema sana ili watu wapate nafasi ya kwenda kushuhudia mechi hii, ndiyo siku ambayo maeneo ya starehe yanayouza vinywaji baridi na moto hupata wateja wengi.

Masikio ya watu wengi huwa na shauku ya kusikiliza sauti ya mtangazaji kwenye redio akitangaza goli. Hapo ndipo tambo huanza.

Tambo ambazo huzaa furaha na huzuni ndani ya hizi timu, hajawahi kutokea shabiki akakubali timu yake ni mbovu mbele ya mpinzani wake ndiyo maana ni kawaida watu kuwekeana nyumba ,pesa kwa ajili ya mechi hii.

Burudani huwa inaendelea hata baada ya msimu kuisha, hapa napo kuna ligi mpya huanza. Ligi ya usajili.

Kipindi hiki huwa tunashuhudia ni nani mwenye msuli mkubwa zaidi ya mwenzake katika kuwania saini ya wachezaji nyota hapa nchini, na ni ngumu kwa mchezaji kukataa ombi la kusajiliwa na hizi timu.

Wengi huamini ndoto yao ya kucheza mpira wa kulipwa huanzia hapa, hivo kukaa kwenye timu hizi huwa ni njia rahisi kwao wao kupanda ndege.

Mwanzoni huja na matumaini mengi ndani yao, huja na nguvu na hasira ya kupigana sana ili kufika mbali, lakini tatizo hufika pale tu wanapokanyaga ardhi ya Kariakoo.

Ardhi ambayo kila wakati kuna mwanga , ardhi ambayo ni ngumu kutambua mchana ni upi na usiku ni upi.Ardhi ambayo imejaa kila aina ya starehe.

Ardhi ambayo imebeba wasichana warembo ambao mkoani ulipotoka hawapo, ndipo hapo nguvu yako ya kupigana hupungua.

Image result for rAPHAEL DAUD

Malengo yako ya kufika mbali kimpira huanza kudidimia na kujiona sehemu uliyopo ndiyo sehemu sahihi, ndiyo maana wachezaji wengi huja pale wakiwa kama nyota sehemu waliyotoka lakini wanashindwa kuonesha kitu walichokuwa nacho huko walipotoka.

Mbeya City msimu uliopita ilikuwa na Raphael Daudi ambaye alikuwa kiungo imara tena uwezo wake ulinakshiwa na ufungaji wa magoli pamoja na utoaji wa pasi za mwisho za magoli

Timu za kariakoo zilimtaka , lakini jangwani ilikuwa sehemu yenye bahati kwake kufikia, lakini tangu afike hajaamka.

Kanogewa na kitanda cha ugenini, hataki kuamka ili atengeneze kesho yake aliyokuwa anaitamani wakati yupo Mbeya City.

Kasi ƴyake iko polepole sana, hana njaa tena, kashiba pesa za usajili hafikirii kupatumia jangwani kama sehemu ya yeye kwenda walipo kina Simon Msuva.

Muda bado anao, hata hajachelewa cha muhimu ni sisi kumkumbusha tu kuwa pale kariakoo kila wakati kuna mwanga ni ngumu kujua kama pamekucha au ni usiku, vazi la utumwa ndilo vazi sahihi kwake ili afanye kazi bila kusubiri jua kuchomoza

Sambaza....