Jana imetoka hukumu ya makamu wa raisi wa TFF, Michel Richard Wambura, ambaye alikuwa anakabiliwa na makosa matatu.
Kosa la kwanza ni kupokea fedha za shirikisho kwa malipo yasiyo halali, kosa la pili ni kughushi barua ya kuelekeza malipo ya kampuni la Jeck system Limited na kosa la tatu ni kushusha hadhi ya shirikisho kwa alichokifanya kwenye makosa namba moja na mbili.
Kuna vitu ningependa tuviangalie kwa pamoja kuanzia jinsi kesi ilivyoanza mpaka hukumu ilivyotolewa.
Michel Richard Wambura anahukumiwa kwa kosa la kwanza ambalo ni kupokea fedha za shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) yasiyo halali. Ukiangali katiba ya TFF iliyofanyiwa mabadiliko mwaka 2013 kwenye kanuni za maadili kifungu cha 73(1) kinamhukumu moja kwa moja Michel Richard Wambura.
Hapa kwa kanuni za kimaadili ya TFF zitakuwa zinamhukumu moja kwa moja Michel Richard Wambura.
Swali la kujiuliza, Michel Richard Wambura amepatikana na hatia ya kupokea pesa za shirikisho kwa malipo yasiyo halali, kosa ambalo kwa mujibu wa sheria za nchi ni kosa la jinai
Jinai nikosa dhidi ya jamhuri. Sheria ya Sura ya 16 ya sheria za Tanzania iliyofanyiwa marejeo 2002 inataja makosa ambayo
ni dhidi ya jamhuri pamoja na adhabu zake.
Sasa jamhuri ni nini? Sheria ya sura ya 16, tajwa humu, katika sura yake ya pili inatoa maana ya Jamhuri kuwa
(refers not only to all persons within Mainland Tanzania but also to the persons inhabiting or using any particular place, or any number of those persons, and also to such indeterminate persons as may happen to be affected by the conduct in respect to which such expression is used), kwa tafasri ya moja kwa moja Jinai ni kosa au makosa yanayofanywa na mtu/watu/taasisi kupitia watendaji wake,kinyume cha sheria au taratibu zilizoainisha makosa mabalimbali. kwa mfano makosa yote yaliyoainishwa katika sheria ya kanuni za adhabu Sura ya 16.
Sasa katika kosa la kwanza la Michel Richard Wambura , ni kupokea fedha za shirikisho ya malipo yasiyo halali, hii moja kwa moja ni kosa la jinai.
Kosa ambalo linatambulika na sheria za nchi kama ilivyoainishwa katika sheria ya sura ya 16, kwanini TFF isiende mbali zaidi kisheria na kumfungulia kesi Michel Richard Wambura katika mamlaka za kisheria za nchi?
Wakati tukijiuliza swali hilo twende tena tukajiulize swali jingine linalotokana na kosa la pili alilopatikana nalo Michel Richard Wambura, kosa la kughushi barua ya kuelekeza malipo ya kampuni la Jeck System Limited yafanyike kupitia yeye. Hii ni kinyume na kanuni za maadili ya TFF, kanuni 73(7) ya kanuni ya maadili ya mwaka 2013
Kosa hili kwa mujibu kwa sheria za nchi ni kosa la jinai, na kosa la jinai linatambulika kisheria kama nilivyoelezea huko juu, kwanini pia TFF Isiende mahakamani ili mahakama itoe adhabu ambayo itakuwa fundisho kwa wengine?
Kosa la tatu na la mwisho kwa mujibu wa kamati ya maadili ya TFFF ni kosa la Michel Richard Wambura ni kushusha hadhi ya shirikisho kwa alichokifanya kwenye makosa namba 1 na 2, hii ni kinyume na kifungu cha 50(1) cha makosa ya jinai.
Katika sheria za nchi kosa hili linachukuliwa kama kosa la “Defamation” ambalo kwa tafsiri ambayo siyo rasmi linajulikana kama “Kudhalilisha”.
Sheria mpya inayojulikana kama sheria ya huduma za habari,2016 (The media services Act, 2016) ambayo imefuta sheria ya Magazeti (The Newspapers Act, No.3 of 1976) imeainisha kosa hili katika SURA YA TANO kama ifuatavyo
“Defamation” ni nini?
Kwa mujibu wa kifungu cha 35 kifungu kidogo cha 1 sheria ya Huduma za habari imefafanua kuwa “ jambo lolote ambalo likichapishwa na kusambazwa linaweza kuharibu hadhi ya mtu, au utu wake au kuibua chuki dhidi yake au kuharibu kazi au fani ya mtu huyo, ni jambo la kudhalilisha”.
Nanukuu: Section 35(1) “any matter which, if published, is likely to injure the reputation of any person by exposing him to hatred, contempt or ridicule, or likely to damage any person in his profession or trade by an injury to his reputation, is defamatory matter”.
Hivyo basi kudhalilishwa ‘Defamation’ ni hali inayojitokeza kwa mtu yoyote pale ambapo jambo la kudhalilisha limechapwa na kusambazwa dhidi yake na kupelekea kuharibu hadhi ya mtu huyo, utu wake au kuibua chuki dhidi yake au hata kuharibu kazi au fani ya mtu huyo. Kwa mujibu wa kifungu tajwa hapo juu mtu yeyote anaelalamika kuwa amedhalilishwa ni lazima ithibitike/athibitishe mbele ya mahakama.
Kimsingi makosa mawili ya mwanzo ya Michel Richard Wambura yamedhalilisha shirikisho la mpira Tanzania ( TFF) pamoja na wapenda mpira, sasa kwanini TFF isichukue tena maamuzi ya kimahakama dhidi ya hii kesi?
Kimsingi TFF kama inajiaminisha kwenye hili inatakiwa iende zaidi ya sehemu ambayo imeishia (kwenye kamati ya maadili) inatakiwa iende kwenye vyombo vya maamuzi ya kisheria vya nchi.
Wakati TFF inavifikiria hicho, Michel Richard Wambura anatakiwa atujibu maswali yafuatayo.
Ni kweli aliomba mkopo wa kifedha kutoka kwa kampuni la Jerkers system Limited bila idhini ya kamati ya utendaji ?
Na kama jibu ni ndiyo kampuni ya Jerkers System Limited linajihusisha na utoaji wa mkopo ?
Sheria za mikopo zinaruhusu taasisi ipi itoe mikopo?
Kwanini malipo yafanyike ƙkipindi ambacho yeye alikuwa madarakani na kipindi ambacho kinachosemekana marafiki zake ( Rais Jamal Malinzi ) walipo kuwa madarakani ? Kwanini ƙkipindi cha Raisi Leodigar Chilla Tenga malipo hayakufanyika?
Ile barua JKC/SONT/TFF/2014 ya tarehe 13/01/2014 inayoonesha Michel Wambura ameidhinishwa na kampuni ya Jeck System Limited , kwanini inakanwa na mke wa marehemu (kwa sasa ndiye msimamizi mkuu wa mirathi) ambaye alikuwa mmiliki wa kampuni hiyo?
Wakati tukisubiri majibu ya Wambura tunatakiwa pia tupate majibu ya TFF kwenye maswali yafuatayo.
Kwa mujibu wa kanuni za maadili namba 48 ya TFF ya mwaka 2013 inaainisha kuwa barua ya wito inatakiwa ipelekwe siku tatu kabla ya siku ya kusikilizwa kwa kesi. Je ni kweli walipeleka barua siku moja kabla ya kesi kusikilizwa, kama ni kweli hawaoni kuwa walifanya makosa kulingana na kanuni za maadili ya TFF ?
Kwa mujibu wa kanuni ya 58 ya kanuni za maadili ya TFF ya mwaka 2013 inaainisha kuwa mtuhumiwa anapofika mbele ya kamati anatakiwa apewe siku za kukusanya ushahidi na mashahidi wa kesi husika, lakini kwa mujibu wa mwanasheria wa Michel Richard Wambura hii kanuni haikufuatwa, tunatakiwa tujue ni kwanini haikufutwa?
Michel Richard Wambura kahukumiwa bila kujitetea mbele ya kamati, kwanini kamati haikumpa nafasi ya kujitetea?
Kuna ufafanuzi wa matumizi ya bilioni 3 ndani ya miezi saba, kuna haja ya TFF kutoka nje na kuonesha matumizi ya pesa hizo kama ni kweli, kama siyo kweli wakanushe kwa kuainisha matumizi ya pesa ndani ya miezi saba ya uongozi wao.
Kaimu katibu mkuu wa TFF ni kiongozi wa chama cha makocha Tanzania TAFCA. Ambapo moja kwa moja kwa mujibu wa kanuni anaingia moja kwa moja kama mjumbe wa kamati kuu ya TFF, ambapo ukiwa mjumbe wa kamati kuu ya TFF hutakiwi kuwa mwajiriwa wa shirikisho la TFF, hivo kaimu katibu mkuu wa TFF anakosa sifa za kuwa mwajiriwa wa TFF, TFF inatakiwa ije mbele yetu na kutudhibitishia Kaimu katibu mkuu yupo kama mtu anayejitolea pale kama ilivyo kwa Afisa Habari ?