Sambaza....

Kocha Ernst Middendorp ameachana na Singida Fountain Gate juzi jioni na jana mchana alikuwa moja ya abiria waliotua katika Uwanja wa ndege wa Afrika Kusini, O. R Tambo.

Ernst hajafikisha hata mwezi ndani ya timu. Sijui kama amepokea hata sehemu ya mshahara wa muda aliofanya kazi. Sababu iliyomfanya aondoke ni kuingiliwa majukumu yake katika mambo ya ufundi. Hizi ndiyo tabia za makocha wanaojitambua zilivyo.

 

Kwanza ni viburi, wanajiamini, hawana cha kupoteza. Ni rahisi kumuingilia majukumu yake kocha asiyejitambua akakaa kimya, lakini kocha anayejitambua maisha lazima yawe tofauti.

Unapaswa kujipanga unapotaka kumuingilia majukumu yake kocha anayejitambua. Sijamshangaa sana Ernst kwa alichokifanya kwa mabosi zake pale Singida Fountain Gate.

Makocha wanaojielewa hawaruhusu upuuzi huu. Katika kilele cha ubora wake Josse Mourinho aliwahi kumchana Roman Abramobic alipokuwa na tabia ya kwenda katika mazoezi ya Chelsea na kutoa ushauri wa mambo ya ufundi.

Jose Mourinho.

Mourinho alisema “Boss jukumu lako ni kututafutia pesa kwa ajili ya kuendesha mambo hapa klabuni, mambo ya ufundi tuachie sisi, hata mimi nikija kukushauri masuala ya biashara utafilisika.”

Tangu siku hiyo, Roman alikata mguu wake kwenda mazoezini. Nae alikuwa anakutana na timu kama mashabiki wengine katika mechi.

Walichokifanya viongozi wa Singida Fountain Gate kwa Ernst huko nyuma kimefanywa sana na viongozi wa mpira wetu.

Ernst Middendorp.

Simba na Yanga zimewahi kutekwa na makundi ya Wanachama yenye nguvu na kufichwa kusikojulikana.

Timu hizi zimeishi maisha haya kwa muda mrefu, kabla ya usasa kuwaingia viongozi wa kileo na kuanza kuziendesha timu Kisayansi.

Singida Fountain Gate wameturudisha kule kwenye dunia nyeusi. Walichokifanya viongozi wao, kina Rashid Ngozoma Matunda na mwenzake Juma Salum wamefanya sana huko nyuma.

Kocha Ernst Middendorp akitambulishwa na viongozi wa Singida Fountaine Gate Fc.

Kwa Juma na Ngozoma kusikia wamemuingilia kocha ampange fulani na asimpange fulani ilikuwa kitu cha kawaida kabisa. Dunia ya leo haya mambo hayako tena.

Timu inaandaliwa na mwalimu, inapangwa na mwalimu, mwisho wa siku ni mwalimu anayewajibika mambo yakienda kombo.

Sambaza....