Wananchi Yanga kesho wanashuka dimbani katika mchezo wa pili wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Maafande JKT Tanzania waliopanda daraja msimu huu.
Yanga watakua nyumbani katika dimba la Azam Complex Chamazi katik mchezo utakaopigwa saa moja kamili jioni. Kuelekea mchezo huo kocha wa Yanga Miguel Gamondi ameongea na Wanahabari akielezea hali ya timu yake kuelekea mchezo huo.
Kuelekea mchezo huo Gamondi alisema “Kuna wachezaji kadhaa waliokumbwa na majeraha mchezo uliopita lakini kwa sasa wapo salama na tayari kuwavaa wapinzani wetu siku ya kesho,” alisema kocha na kuongezea;
“Kuhusu Skudu ameshaanza mazoezi ya gym jana na wiki hii tutamweka kwenye uangalizi kisha baada ya hapo ataanza mazoezi na wachezaji wenzake.”
Muargentina huyo pia ameelezea hali ya kikosi chake lakini pia amelalamikia ratiba ya Yanga akisema wanacheza michezo inayofuatana mno na kuwachosha wachezaji lakini hakuonyesha kuibeza JKT licha yakwamba ndio kwanza imepanda daraja.
“Mimi sipendelei kusema mchezaji yupi atakuwepo au yupi hatakuwepo, kikubwa hali za wachezaji wetu zipo sawa, tumekuwa na ratiba ngumu kidogo baada ya kucheza mechi 3 ndani ya siku 10, tena kwenye viwanja vya nyasi bandia, viwanja vya nyasi bandia sio vizuri sana husababisha majeraha kwa wachezaji lakini uzuri ni kwamba wachezaji wetu wote wapo salama.”
“Licha ya kwamba mpinzani wetu tunajua ni timu iliyopanda daraja, najua kwamba wana wachezaji wenye uzoefu kwenye ligi hivyo hatupaswi kuichukulia kama timu dhaifu au ngeni kwenye ligi. NI wageni kwa maana ya timu lakini wana idadi kubwa ya wachezaji wenye uwezo lakini sisi ni timu kubwa na tupo nyuma nafikiri kesho tunapaswa kujiamini na kufunga magoli mengi,” alimaliza Gamondi.