Wapwa, kisa cha “maji kupwa maji kujaaa” kwenye mchezo wa Kaizer Chief baada ya kuingia akitokea benchi Crispine Ngushi alionesha kitu watu tukadhani amezaliwa upya.
Jana wakati anaingia mimi nilifurahi sana kuona kijana ameaminika mbele ya mafundi kadha wa kadhaa waliokuwa nje hasa Aziz Ki, mpwa wangu mwenyewe Sure Boy na wengine wengi.
Nikajua ‘runinga’ imewaka nikajiuliza maswali na nikajipa jibu moja tu hii ndiyo ile ya kunufaika anapokuja kocha mpya basi kuna baadhi ya wachezaji walikuwa hawapati nafasi watapa na wale waliokuwa wanapata nafasi watakosa kutokana na mahitaji katika filosofia yake.
Binafsi kwa akili yangu nilidhani Aziz Ki atakuwa wa kwanza kwenye yale mabadiliko kisha akaenda kwenye nafasi ya namba 10 huku Farid akienda pembeni na kiungo wa kushoto kuziba nafasi ya Skudu Makudubela moja kwa moja.
Nilichokiona ni kupania vilivyo mechi ile kwa Ngushi kutaka kutusuta siye wenye maneno mingi, kumuonesha mwalimu miye nastahili kuanza kikosi cha kwanza mwishoe akashindwa kufanya vyema kabisa.
Athari ya jambo hili ni kubwa kuliko unavyodhani kurudisha tena imani kwa benchi la ufundi ni shughuli pevu sana na bahati mbaya sana walioingia akiwemo aliyechukua nafasi yake akafanya vyema.