Kikosi cha Simba kimecheza michezo mitatu ya kirafiki kikiwa nchini Uturuki katika maandalizi ya msimu huku kocha wake akisema vijana wameiva na kuhitaji mchezo mmoja mwingine kabla ya kurudi nchini.
Kikosi cha Wekundu wa Msimbazi kimejichimbia nchini Uturuki kujiandaa na michuano ya Kitaifa na Kimataifa lakini kubwa zaidi ni michuano mipya ya Super Cup ambapo itaanza kutimua vumbi Barani Afrika kwa mara ya kwanza mwaka huu.
Ikiwa nchini humo tayari Simba imecheza michezo mitatu ambapo walifungwa bao moja bila dhidi ya Zira fc kabla ya kucheza michezo miwili kwa siku moja dhidi ya Turan PFK. Katika michezo hiyo mchezo wakwanza Simba ilishinda mbili bila kabla ya mchezo wa pili kupoteza kwa bao moja bila.
Baada ya michezo yote hiyo kumalizika Robertinho alisema “Kwangu siangalii matokeo ya mwisho bali mchezo wenyewe ulivyokuwa. Tumecheza vizuri kuanzia mwanzo hadi mwisho.”
“Wachezaji wameonekana wapo timamu kimwili, kimbinu na hilo ni jambo ambalo limenifurahisha. Nawapongeza pia wasaidizi wangu wamefanya kazi kubwa kwa muda mfupi,” alisema Mbrazil huyo.
Kikosi cha Simba kinatarajia kurudi nchini mapema August moja ambapo wanajiandaa kucheza mchezo wa kirafiki wa Kimataifa dhidi ya Power Dynamos ya Zambia katika kilele cha Simba Day.
Wakiwa nchini humo tayari kocha Robertinho amepata fursa ya kuwaona wachezaji wake wote wapya baada ya kucheza michezo hiyo ya kirafiki. Klabu ya Simba imesajili wachezaji kumi wapya, wanne wazawa na sita wakigeni.