Sambaza....

Aliyekua kocha mkuu wa Yanga Nasraddine Nabi anatarajiwa kuchukua nafasi ya Mohammed Aziz Samadi, ambaye aliiongoza AS FAR kutwaa ubingwa wa Morocco wiki mbili zilizopita kama kocha wa muda.

Samadi, nguli wa klabu ya FAR, alishikilia jukumu hilo baada ya kikosi cha jeshi kumfuta kazi kocha mkuu Fernando Da Cruz. Da Cruz alionyeshwa mlango wa kutokea baada ya klabu hiyo kutolewa kwenye Kombe la Klabu Bingwa ya Kiarabu.

Wakati huo huo FAR “Jeshi Jeusi” lilichukua hatua haraka yakuanza kuingia makubaliano na Nabi  ambayo yanaweza kumfanya awaongoze katika msimu ujao. Kama mambo  yatakwenda kama yalivyo klabu inaweza kutangaza uteuzi wake mapema wiki ijayo.

Nasraddine Nabi.

“Nabi ni kocha mwenye uzoefu mkubwa na rekodi ya mafanikio iliyothibitishwa. Ameshinda mataji nchini DR Congo na Tanzania, na klabu ina imani kuwa atakuwa na thamani kubwa kwa klabu,” chanzo kiliiambia FAR Post.

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 58 ataiongoza klabu hiyo kutetea taji linalotamaniwa la Botola Pro. Kocha huyo wa Tunisia ana uzoefu mkubwa katika soka la Afrika. Amewahi kuzifundisha Al Merreikh ya Sudan, AC Leopards ya DR Congo, Ismaily SC ya Misri na Yanga.

Nabi anajulikana kwa mtindo wake wa uchezaji wa kushambulia na anatarajiwa kuleta mwelekeo mpya katika mashambulizi kwa timu hiyo ya jeshi. Mara baada ya Nabi kutambulishwa rasmi, basi ataanza kazi ya kuandaa timu kwa ajili ya msimu mpya.

Sambaza....