Sambaza....

Mabingwa wa ligi kuu bara Yanga SC wamefungiwa kusajili wachezaji na shirikisho la soka duniani FIFA. Katazo hilo limekuja baada ya shirikisho la soka duniani kuikuta Yanga na hatia ya kutotimiza masharti ya kifedha kwa kocha wake wa zamani, Luc Eymael.

Katika taarifa hiyo kutoka FIFA ilisema “Tunatambua kuwa katika mawasiliano yake, mdai anatufahamisha kuwa mlalamikiwa, klabu ya Young Africans SC, hajatekeleza wajibu wake wa kifedha kwa mujibu wa uamuzi wa FIFA,” ilisomeka barua iliyosainiwa na mratibu wa nidhamu wa FIFA, Pablo. Arias.

“Kuhusu hili, tunapenda kuzifahamisha vyama kuwa marufuku ya kusajili wachezaji wapya kimataifa imetekelezwa na FIFA kuanzia leo.”

Luc Aymael aliyekua kocha mkuu wa Yanga sc.

“Aidha, kwa mujibu wa uamuzi huu uliotajwa hapo juu, chama cha soka nchini Tanzania (TFF) kinaombwa kutekeleza mara moja kwa mlalamikiwa, Young Africans, marufuku ya kusajili wachezaji wapya katika ngazi ya Taifa.”

Katazo hilo limekuja baada ya FIFA, Oktoba 2022, kuwaamuru vigogo hao wa Tanzania, kumlipa aliyekuwa kocha wao Eymael dola 148,000 (TSh346 milioni) kwa kufukuzwa kazi isivyostahili.

Sambaza....