BONDIA wa ngumi za kulipwa nchini, Seleman Kidunda amewaomba mashabiki wake kujitokeza kwa wingi Juni 30, mwaka huu katika Ukumbi wa Mlimani City ili kuweza kushuhudia atakavyompiga mpinzani wake Eric Mukadi kutoka DR Congo.
Kidunda ametoa kauli hiyo kuelekea katika pambano hilo liliandaliwa na Kampuni ya Promosheni ya ngumi za kulipwa nchini PAF Promotion Company Limited huku pambano hilo likipewa jina la Hata Usipolala pata kucha ambapo pia Mfaume Mfaume ‘Mapafu ya Mbwa atapanda ulingoni dhidi ya Nkululeko Mhlongo wa Afrika Kusini.
Kidunda anasema kuwa kwa upande wake yeye amekuwa akiendelea na maandalizi ya kujiandaa ya pambano hilo huku akikataa kuongelea ujumbe wa maneno aliyotumiwa na mpinzani wake kwa kuwa mikakati yake ni kuona anamchakaza vibaya katika pambano hilo.
“Nataka ni kwambie kwamba namshukuru Mungu, naendelea na maandalizi ya pambano kwa kufanya mazoezi makali kwa sababu najua halitokuwa pambano jepesi kutokana mpinzani mwenyewe, maneno yake hayawezi kunitisha na nisingependa kuongelea anachokisema zaidi ya mimi kujikita kwenye maandalizi kwa sababu atakavyokuja ndiyo tukakavyompokea.
“Kwa nini isiwe rahisi? unajua ubora wangu na ninavyokuwa kwenye ringi (ulingo) sasa kwa nini asipigike kama nafanya mazoezi kwa ajili yake! Lakini ninachotaka kuwaambia kwa sasa mashabiki wangu waje kwa wingi Mlimani City hiyo Juni 30, nataka waje waangalie burudani ya ngumi na siyo maneno kama anavyosema mpinzani wangu, ” alisema Kidunda.
Mapambano mengine ya utangulizi yatakuwa kati bondia Fadhili Majiha ‘Stopper’ atakayepanda ulingoni dhidi ya Jamal Kunoga wakati Saleh Kasim atamalizana na Said Bwanga kabla ya Deo Samweli kumvaa Adam Ngange.
Wengine ni Pius Mpenda ambaye atapanda ulingoni dhidi ya Simon Tichecha wa Malawi wakati Rama Jonh Cina akitarajia kupasuana na Yona Segu lakini Omary Maulid atapanda na Shaban Kibiriti na Boniface Seguda atacheza na Hamza Mahamoudu huku Herry Rashid akitarajia kumalizana Hussein Pendeza.