Katika kilele cha ubora wake Athuman Iddy Chuji kiwanjani aliwaambia Simba yuko radhi aende gengeni kuuza Ndimu sio kucheza Simba. Hapa Athuman alikuwa wa moto kweli kweli. Kila alichokuwa anaufanya mpira, mpira ulimtii.
Baada ya kauli hii ya kibabe, miezi kadhaa baadae, picha za Athuman zilionekana akitambulishwa kama mchezaji mpya wa Simba. Awamu hii Athuman hakuwa tena yule.
Nyakati zimekwenda zake sasa. Athuman amestaafu soka la ushindani. Hayuko tena kiwanjani. Siku hizi ni kocha wetu katika timu yetu ya mtaa. Wakati ni ukuta.
Nimemkumbuka rafiki yangu Athuman niliposikia mahojiano ya Feisal Salum na kituo cha Clouds Fm jana. Feisal ametapika nyongo.
Hofu yangu ni moja, anaweza kukisimamia kile alichokisema? Hofu yangu inaanzia hapa. Shida ya wachezaji wetu sio wa kuwaamini sana katika matamshi yao. Leo atasema hivi, kesho atasema vile. Mifano iko mingi kwa wachezaji tofauti tofauti.
Feisal amemaliza maneno jana. Hajaweka Nukta, koma wala mkato. Kama kitabu amemaliza kukiandika hadi kurasa ya mwisho. Hana alichokibakisha.
Nafahamu watu wa visiwani wanaamini katika wanachokiamini. Ni ngumu kuwatoa katika anachokiamini, hofu yangu inakuja Feisal ni mchezaji. Wachezaji wengi wanafanana mambo yao.
Kama Athuman tunayeamini ni mtu mbishi, mhuni, alilamba matapishi yake mchana kweupe kwa kusaini Simba, vipi Feisal na Yanga pamoja na Rais wake Hersi Said?
Natamani kuona mwisho wa Feisal na Yanga utakavyokuwa. Mpaka sasa inaonyesha hautakuwa mwisho mwepesi mwepesi, lakini usiwaamini sana wachezaji.
Kuna wachezaji wachache wanaoweza kusimamia kile wanachokisema hadi mwisho, lakini wengi wakiitwa katika vikao vya Sambusa, Korosho wanayameza maneno yao. Wacha tuone mwisho wa Feisal na Yanga utakuwaje.