Sambaza....

Nasikia Simba wanataka kupitisha panga kubwa la wachezaji wazawa kikosini mwao. Good. Naheshimu katika wanachokiwaza, lakini Simba wanaamini sokoni kuna mchezaji wa kizawa anayeweza kuja kuingia kikosi chao cha kwanza cha msimu ujao?

Ninachokiona wanachotaka kukifanya ni kuwabadili wachezaji wa zamani wa benchi, kisha waje wapya wengine wa benchi. Hiki ndicho ninachokiona na kitakwenda kutokea.

Mahitaji ya timu zetu kubwa mbili yameongezeka kwa kiwango kikubwa. Soka letu halina tena mchezaji wa kizawa anayeweza kuingia kikosi ya kwanza cha Simba na Yanga moja kwa moja kwa hawa wanaocheza NBC Premium League. Kama tuko nitajie jina lake.

Jonas mkude akimnyanyasa kiungo wa Al-Ahly katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Nini kinachopaswa kufanyika sasa juu ya wachezaji wazawa wa Simba? Wasainishwe mikataba migumu. Usipocheza asilimia fulani ya michezo unakatwa pesa. Hii inafanyika katika timu nyingi za wenzetu.

Mazingira yaliyoko sasa hayamfanyi mchezaji wa kizawa kujiona ana deni na anapaswa kulilipa kwa kumwagika jasho. Wengi wanajiona wako katika sehemu salama wakitoka kusaini mikataba minono yenye fedha na funguo za gari mezani.

Mchezaji wa kizawa unayeamini ukimuacha anakwenda kupata nafasi ya kucheza katika timu nyingine, kisha mzawa unayemleta anakuja kuishia benchi, unamuachaje mchezaji wako mzawa wa zamani?

Muwekee tu mazingira mazuri. Mchezaji huyu hupaswi kumuacha, maana sokoni hakuna mwingine anayeweza kukupa kitu kipya. Weka tu mikataba migumu kisha muache afanye kazi.
Muda utakuja kumuhukumu mchezaji husika. Lakini kinachotaka kufanyika sasa ni Iddy kutaka kumuita Idrisa.

Sambaza....