Siku Jumatano Yanga Sc wanakwenda kucheza mchezo wa kwanza wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya timu ya Marumo Gallants ya Afrika Kusini, mchezo huo utachezwa majira ya saa 10:00 za jioni kwa saa za Afrika mashariki.
Marumo Gallants ni timu inayotokea nchini Afrika Kusini katika mji wa Limpopo na ilianzishwa mwaka 2001 na kwa mara ya kwanza ilishiriki Ligi kuu ya nchi hiyo msimu wa 2021/2022 na kushika nafasi ya 10 huku pia wakifika fainali ya kombe la Nedbank na kupata nafasi ya kushiriki kombe la Shirikisho Afrika.
Marumo Gallants imekuwa na matokeo ya kustaajabisha kwani kwenye ligi ya nchini kwao haifanyi vizuri lakini inapokuja swala la Kombe la Shirikisho Afrika wamekuwa na matokeo mazuri zaidi.
Marumo licha ya kumaliza vinara wa kundi A lililokuwa na timu za USM Alger ya Algeria, Saint-Eloi Lupopo ya DR Congo na Al Akhdar ya Libya, wakiwa na pointi 12 baada ya mechi 6, ni timu ambayo inafungika na inaruhusu mabao mengi kwani ilimaliza ikiwa imefunga mabao 12 na kufungwa mabao 10.
Ilifungwa mabao 4-1 na Al Akhdar kule Libya na ikapasuka 2-0 ugenini dhidi ya USM Alger, lakini ikaja kulipa kisasi kwa kushinda 4-1 dhidi ya Al Akhdar na kushinda pia 2-0 dhidi ya USM Alger. Maana yake hii ni taa nyekundu kwa Yanga kwamba hata ikishinda kwa mabao manne Kwa Mkapa isije kushangilia sana na kudhani kuwa mechi imeisha kwa sababu Gallants wana uwezo wa kukufunga kwao kama ulivyowafunga kwako.
Timu hiyo ambayo kwenye Ligi ya PSL inashika nafasi ya tatu kutoka mkiani ikiwa na pointi 29 baada ya mechi 28, imefungwa mabao 30 huku yenyewe ikifunga mabao 27 tu, lakini ni timu inayocheza kwa staili ya piga nikupige kwani katika moja ya mechi zake za makundi ya Shirikisho msimu huu ilishinda 3-2 dhidi ya Lupopo.
Jambo la kuchunga ni kwamba Marumo ni wakali sana kwenye uwanja wa nyumbani, wameshinda mechi zote nne hadi kufikia sasa kwa jumla ya mabao 10, hawajapoteza mchezo wala kutoa sare katika Kombe la Shirikisho msimu huu.
Yanga ambayo ilimaliza kinara wa Kundi D ikiwa na pointi 13, moja tu zaidi ya Marumo, ilifunga mabao tisa na kuruhusu manne, ikiwa timu iliyofungwa mabao machache zaidi msimu huu (manne) sawa na Asec Mimosas ambayo pia iko nusu fainali na US Monastir, ambayo ilikwamia kwenye robo fainali.
Marumo inacheza kitimu, lakini ina watu muhimu zaidi ambao wanaifanya ilete shida kwa wapinzani na mmoja wao ni straika wao, Ranga Chivaviro, ambaye amekuwa kwenye kiwango bora katika michuano hii kwani ndiye kinara wa mabao wa Shirikisho msimu huu, akilingana na Fiston Mayele wa Yanga, kila mmoja akiwa na mabao matano.
Wakati kina Bakari Mwamnyeto na Ibrahim Bacca, wakiandaliwa kumdhibiti Rango Chivairo wapo watu wengine ambao ni hatari katika kumtengenezea nafasi na pia kutoa pasi za mabao kuna kiungo kama Lesiba Nku ambaye amechangia mabao matatu akifunga mawili na kutoa pasi moja ya goli katika Kombe la Shirikisho mpaka sasa.
Hao ndio Marumo Gallants fc timu inayo inataka kuandika historia mbele ya Yanga sc na Yanga sc wanataka kuandika historia kupitia wao.
Imeandaliwa na Abuu Mwakyoma