Fiston Kalala Mayele ameendelea kuandika jina lake katika historia ya klabu ya Yanga kutokana na rekodi yake nzuri ya mabao anayoendelea kuiandika mpaka sasa akiwa na Wananchi.
Baada ya kufunga mabao mawili katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Rivers United hapo jana sasa Fiston Mayele amefikisha mabao 50 akiwa na jezi ya Wananchi Yanga.
Fiston ametumia misimu miwili pekee akicheza mechi 75 kuweza kufikisha idadi hiyo ya mabao akiwa na Yanga huku ikitegemewa kuendelea zaidi kutokana na kasi yake ya upachikaji wa mabao pamoja na idadi ya mechi za Yanga zilizobaki msimu huu.
Nyota huyo wa zamani wa AS Vita aliyejiunga na Yanga August 2021 katika msimu uliopita pekee alifanikiwa kufunga mabao 20 likiwemo bao moja alilofunga katika mchezo wake wa kwanza wa mashindano dhidi ya Simba katika mchezo wa Ngao ya Jamii.
Kwa msimu huu peke nyota huyo kutoka Congo ameshafunga mabao 30 huku akiwa na nafasi ya kuongeza mengine kwa msimu huu kwani mpaka sasa Yanga wana mechi nne za Ligi Kuu pia wakiwa nusu fainali ya FA pamoja na robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Mayele ambae huenda msimu huu ukawa wamwisho kwake kuwatumikia Wananchi amesema “Ni rekodi ambayo tunaifanya kwa pamoja nawashukuru wote viongozi hasa Rais Hersi, benchi la ufundi kwa kuniamini na kazi nzuri ya maboresho, wachezaji wote kwa kujiamini na support ya mke wangu ambaye amekuwa akiniunga mkono katika mipango yote. Mwananchi andika sasa kwenye comment goli pendwa kati ya 50,” alimalizia Mayele.
Katika Ligi Kuu ya NBC mpaka sasa Mayele ana mabao 16 ba kumfanya kuwa kinara wa mabao wakati katika FA ana bao moja pekee na katika Kombe la Shirikisho Afrika ana mabao matano.
Fiston sasa ni kama Yanga wamepata mshambuliaji wa kariba yake kwani misimu kadhaa nyuma wamekua katika ukata mkubwa kupata mshambuliaji wa maana. Wamepita kina David Molinga, Yikpe Ayigben, Michael Sarponga na Juma Balinya lakini hawakuwa bora kama ambavyo Mayele anafanya sasa.