Tayari Wananchi Yanga wapo nchini Nigeria kuelekea mchezo wao wa robo fainali dhidi ya Rivers United na leo wamefanya mazoezi yakiufundi wakiwa nchini humo wakiwa na viongozi wao wa juu wa klabu.
Rais wa klabu ya Yanga Injinia Hersi Said amesema licha ya kupoteza mchezo dhidi ya Simba lakini bado mashabiki wao wanaamini watawafurahisha katika michuano ya Afrika.
“Mashabiki wana imani kubwa sana na nyie, tumepoteza derby lakini bado wamekua sambamba na nyie kwasababu wanaamini mnakwenda kuwapa rekodi ya kucheza nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika,” alisema Hersi Said
Kikosi cha Yanga leo kimefanya mazoezi katika uwanja wa Akwa ambapo walitumia takribani dakika 90 kujiandaa na mchezo huo utakaopigwa siku ya Jumapili mchana kwa saa za Nigeria wakati huku kwetu Tanzania itakua ni saa kumi jioni.
Yanga watashuka dimbani wakiwa na mpango wa kutopoteza mchezo huo ama kupoteza kwa tofauti ndogo ya mabao kwani wana faidi ya kumaliza mchezo wa pili nyumbani ambapo watarudiana na Rivers United wiki moja baadae katika Dimba la Benjamin Mkapa
Wananchi wana kila sababu yakuandika historia mpya yakutinga nusu fainali ya michuano ya Shirkisho Afrika kutokana na kikosi walichonacho lakini pia faida ya kuanzia ugenini.