Sambaza....

Kuelekea mchezo wa robo fainali kati ya Simba na Wydad Casablanca Wekundu wa Msimbazi Simba tayari wametaja viingilio katika mchezo huo ambao wanakwenda kusaka rekodi ya kucheza nusu fainali baada ya kucheza robo fainali mara kadhaa.

Akizungumza na waandishi wa habari msemaji wa Klabu ya Simba Ahmed Ally amesema kutakua na viingilio vya bei ya kawaida na kama kawaida vifurushi maalum vya tiketi vitakuepo.

“Tiketi tayari zimeanza kuuzwa. Kiingilio cha chini ni Tsh. 5,000 na kiingilio cha juu itakuwa ni Tsh. 30,000. Kutakuwa na vifurushi maalumu kama Mnyama Package hii ni kwa marafiki, vikundi na haina idadi ya tiketi. Kutakuwa na namba ya kupiga kununua,” alisema Ahmed Ally

Wachezaji wa Simba wakishangilia na mashabiki wao baada ya ushindi mnono dhidi ya Horoya.

Ahmed pia amesema wanakwenda kukutana na timu kubwa hivyo mchezo utakua mkubwa na wakuvutia Afrika lakini wao kama Simba wana jambo lao kuelekea nusu fainali.

Ahmed Ally “Mechi ya Simba na Wydad ndio mechi kubwa barani Afrika wiki hii sababu tunakutana na bingwa mtetezi lakini pia watu wanataka kuona Mnyama akivunja historia ya mwaka 2003 kumtoa bingwa mtetezi,” alisema na kuongeza

“Wydad tunaenda kumfanyia balaa, hawataamini. Dhamira yetu ni kuvunja mwiko wa kuishia robo fainali, kumtoa Wydad. Tunakiri wametuzidi ubora lakini tunaamini tunakwenda kuwatoa. Safari hii tunaitaka nusu fainali.”

Wydad Casablanca wapinzani wa Simba katika robo fainali.

Mchezo huo utaangukia katika sikukuu ya Eid hivyo Wanasimba wamealikwa Benjamin Mkapa ili wakale pilau la sikuu na kuona jinsi Simba wanavyotimiza jambo lao mbele ya timu kubwa na bora Afrika.

“Furaha ya Wanasimba haijakamilika, wanatudai nusu fainali. Tunawaomba Wanasimba tushikamane, pamoja na ubora alionao Wydad lakini tukisimama kama Simba hakuna linaloshindikana.”

“Lazima tukawaadhibu Wydad, lazima tuwaonyeshe yaliyomo yamo. Itakuwa ni siku ya Eid siku hiyo, njoo umeshiba pilau lako, umewaka uje tuhakikishe Wydad wanakaa.” alimalizia Ahmed Ally msemaji wa klabu ya Simba.

 

Sambaza....