Sambaza....

Mkuu wa idara ya habari ya klabu ya Simba amesema wao kama Simba pamoja na mashabiki wao wamepata funzo kwa jinsi ambavyo mashabiki wa Al Ahly walivyofanya kuelekea mchezo wao dhidi ya Al Hilal.

Kuelekea katika mchezo huo wa mwisho wa Ligi ya mabingwa Afrika ambao Ahly lazima washinde ili kusonga mbele mashabiki wake wamenunua tiketi zote za mchezo huo ndani ya masaa matatu tu. Ahmed Ally amesema kuna la kujifunza katika jambo hilo.

 

“Tiketi za mchezo kati ya Al Ahly na Hilal ziliisha ndani ya saa 3 baada ya kuanza kuuzwa. Hapa kuna kitu wana Simba tunapaswa kujifunza na mimi semaji lenu ni jukumu langu kuchukua elimu na kuwafikishia ili tuendelee kuboresha eneo letu la ushabiki,” alisema Ahmed Ally kupitia ukurasa wake wa instagram.

Kwasasa Al Ahly haifanyi vizuri na imeonyesha kusuasua katika hatua ya makundi katika Ligi ya Mabingwa lakini mashabiki bado hawajaicha timu yao.

Ahmed Ally “Al Ahly wapo kwenye wakati mgumu, timu yao imesusua kwenye group stage. Lakini hatma yao ya kwenda Robo Fainali ipo mikononi mwao endapo wakishinda dhidi ya Al Hilal. Kwa namna Al Ahly ilivyosuasua mashabiki wenye roho ndogo wangekata tamaa. 

Al Hilal waliibuka na ushindi wa bao moja bila dhidi ya Al Ahly katika mchezo wa kwanza uliopigwa Sudan

Lakini mechi ya mwisho ndo mechi ya kuamua hatma yao hivyo mashabiki wamechukua jukumu la kuisaidia timu yao kwenda Robo Fainali.”

Msemaji huyo wa klabu ya Simba ameongeza kuwa mashabiki wametambua nguvu yao na hivyo ni wazi hata Al Hilal wenyewe wameshtuka kuelekea mchezo huo kutokana na jinsi ambavyo Ahly wamejiandaa.

“Mashabiki wametambua nguvu yao katika mchezo huu na wametambua kuwa hiki ndo kipindi timu yao inawahitaji zaidi Uwanjani.
Ndo maana wamenunua tiketi kwa wingi tena ndani ya muda mfupi.

Ahmed Ally msemaji wa klabu ya Simba Sc.

Nina uhakika Al Hilal wameshtuka kusikia tiketi Elfu 50 zimeuzwa kwa saa 3 hapo tayari wamepata ujumbe kuwa tunakoenda ni pagumu watu wamedhamiria ubaya. Wanangu wa Simba Sports tuishi humu kwamba kwenye nyakati ngumu ndo tunapaswa kuja kwa wingi Uwanjani,” alimalizia Ahmed Ally.

Jumamosi Al Ahly watakua nyumbani wakiwakaribisha Al Hilal kutoka Sudan ambapo Ahly wanahitaji ushindi pekee ili kuvuka na kwenda robo fainali wakati vijana wa Ibenge Al Hilal wao wanahitaji angalau hata sare tu katika mchezo huo.

Sambaza....