Kikosi cha KMC FC kimewasili salama Turiani mkoani Morogoro kwa ajili ya mchezo wa michuano ya Kombe la Azam Sport Federation ASFC utakaochezwa hapo kesho saa 16: 00 jioni katika uwanja wa Manungu Mkoani hapa.
Kocha Mkuu Thierry Hitimana amesema kuwa baada ya kumaliza mchezo wa Ligi Kuu ya NBC soka Tanzania Bara dhidi ya Azam FC , amekuwa na muda wa siku tatu kufanya maandalizi ya mchezo huo na kwamba hali ya kikosi iko vizuri na kila mmoja yupo tayari kutumika kwa ajili ya kuhakikisha kwamba kama Timu inapata nafasi ya kuendelea na michuano hiyo.
Kocha Hitimana ameongeza kuwa anafahamu ugumu wa michuano hiyo na kwamba anaiheshimu Timu ya Mtibwa Sugar kutokana na kwamba imekuwa ni mechi ngumu pindi zinapokutana lakini kama Manispaa ya Kinondoni itakwenda kupambana kuhakikisha kwamba inapata matokeo mazuri na hivyo kuendelea na michuano hiyo.
“Michuano hii ni 50 kwa 50 kwamba hakuna Timu ambayo inauhakika hivyo kila mmoja ananafasi ya kujipanga vizuri uwanjani, tumeshajitayarisha vizuri tunamuomba mwenyezi Mungu azidi kuwapa Afya njema wachezaji wetu ili wakapate kutumika vizuri hapo kesho,” alisema Hitimana.
Kocha Hitimana ameongeza kuwa “Kwenye mchezo huo tutamkosa Davidi Kisu Mapigano, Baraka Majogoro pamoja na Kelvin Kijili kutokana na sababu za majeraha, wengine waliobaki wapo kwenye hari nzuri na morali nzuri , kwani hata kwenye michezo iliyopita walicheza vizuri tofauti ni hatukupata matokeo rafiki.”
Kwaupande wake Nahodha wa KMC FC Sadalah Lipangile amesema kama wachezaji wanatambua umuhimu wa mchezo huo huku akiwasihi mashabiki kutokukata tamaa kwasababu bado wana nafasi ya kufanya vizuri kwenye mchezo wa kesho pamoja na ile ya Ligi Kuu ya NBC licha ya kuwa na changamoto ya matoke yasiyo ridhisha.
Sadalah ameongeza kuwa kipindi hiki kama wachezaji wameweka mikakati madhubuti kwa ajili ya Timu na kwamba kikubwa mashabiki wazidi kuwasapoti pindi wanapokuwa uwanjani kwani uwepo wao unaongeza hari zaidi pindi wanapokuwa wakicheza.