Sambaza....

Na Ibrahim Mussa

MABONDIA Tony Rashid wa Tanzania na Sabelo Ngabinyana kutoka Afrika Kusini jana wamefanikiwa kupima uzito tayari kwa pambano la kuwania mkanda wa Ubingwa wa Afrika katika uzani wa Super Bantam katika pambano linalotarajia kupigwa leo Ijumaa kwenye Ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar.

Tony atapanda ulingoni katika pambano hilo kutetea mkanda wake wa Ubingwa wa Afrika ABU ambao alishinda mwaka jana kufuatia kumchapa kwa pointi Bongani Mahlangu wa Afrika Kusini.

Tony ambaye ni bondia namba moja nchini atetea mkanda huo katika pambano hilo ambalo limeandaliwa na Kemmon Sports Agency huku likitarajia kuwa na upinzani mkali.

Mara baada ya kupima uzito, Tony alisema kuwa amejiandaa vizuri kuhakikisha anafanikiwa kushinda pambano hilo huku akimtaka mpinzani wake kufanya kazi kweli ulingoni kwakuww amemuandalia kichapo kizito katika pambano la leo Ijumaa.

“Nimeajiaandaa vizuri kuweza kushinda pambano lakini kama kweli ametoka Afrika Kusini aweze kuchukua mkanda wangu basi anatakiwa kufanya kazi ya ziada, mashabiki zangu na Watanzania wajitokeze kwa wingi pale Ubungo Plaza, ” alisema Rashid.

Lakini kwa upande wa Sabelo alisema amejiandaa kuondoka na mkanda huo huku akisisitiza hawezi kuwa muongeaji kwa kuwa matarajio yake ni kuweza kushinda.

Wakati huohuo Seleman Kidunda ameshindwa kutokea katika zoezi la kupima uzito huku mpinzani wake Patric Mukala akimtaka ajitokeze leo kumaliza ubishi wao.


Sambaza....