BONDIA wa ngumi za kulipwa nchini, Patric Mukala anatarajia kutua nchini leo Jumanne usiku tayari kwa pambano lake la kuwania mkanda wa Ubingwa wa Afrika ABU katika uzani wa Super Middle dhidi ya Mtanzania, Seleman Kidunda.
Mukala ambaye atacheza pambano kuu dhidi ya Kidunda katika pambano hilo linalotarajia kupigwa Februari 24, mwaka huu kwenye Ukumbi wa Ubungo Plaza sambamba na Tony Rashid atakayepanda ulingoni kutetea mkanda wake wa Ubingwa wa ABU dhidi ya Sabelo Ngabinyana wa Afrika Kusini.
Akizungumza na Spoti Xtra, Promota wa pambano hilo kutoka Kemmon Sports Agency Saada Salum alisema kuwa Mukala na jopo lake la ufundi wanatarajia kutua nchini usiku wa leo Jumanne wakitokea Afrika Kusini tayari kwa pambano hilo.
“Mpinzani wa Seleman Kidunda, Patric Mukala tunatarajia kumpokea Jumanne (leo) muda wa saa moja akitokea Afrika Kusini kwa kutumia Ndege ya Kenya Air ways ‘KQ’ tayari kwa vita yake ya kuwania mkanda wa ABU dhidi ya Kidunda lakini pia mpinzani wa Tony Rashidi.
“Kama tulivyoowaambia awali kwamba Kemmon Sports Agency tumejipanga kuleta Mapinduzi katika mchezo wa ngumi hivyo tunaomba waendelee kununua tiketi katika vituo ambayo vimekuwa zinauza ambazo zinapatikana kwa bei ya shilingi 10,000 , Shilingi 20,000 na Shilingi 50,000 kwa VIP A,” alisema Salum.