Sambaza....

Msimamo wa Kundi F katika Michezo ya kufuzu fainali za Mataifa Huru Afrika AFCON 2023, Unaonyesha Tanzania Ipo katika Nafasi ya tatu ikijikusanyia alama 1 baada ya kufungwa mechi Moja na kutoka Sare Moja.

Tanzania iko chini ya Algeria inayoongoza kundi ikiwa na alama 6 baada ya kushinda mechi 2, kisha Niger katika Nafasi ya Pili ikiwa na Alama 2 baada ya kutoa sare katika michezo yote miwili.

Tanzania bado ina mechi nne ili kujua hatma ya Ushiriki wake katika fainali za mataifa huru Afrika. Mechi hizo ni dhidi ya Niger Nyumbani, kisha Uganda Nyumbani, Algeria Ugenini; huku Mchezo dhidi ya Uganda Ukisubiri kupangiwa tarehe nyingine baada ya kuahirishwa kuchezwa September 19 mwaka huu.

Hiyo ndio michuano pekee ambayo Tanzania kama taifa inaiangalia kwa timu ya wakubwa, hii ni baada ya kushindwa kufuzu Kombe la Dunia bila kusahau kushindwa kufuzu Michuano ya Chan. Mafanikio makubwa kwa Tanzania kwa Miaka ya Hivi karibuni ni Kufanikiwa kufuzu AFCON mwaka 2019 wakati wa Mnigeria Emmanuel Amunike kama Kocha Mkuu.

Kuanzia hapo; Tanzania kwa kupitia timu yetu ya taifa hatukupa mafanikio yanayoweza kuwa kama alama muhimu katika historia ya Soka nchini. Hii si kwa bahati mbaya bali ni kutokana na hali ilivyo na jinsi mambo yanavyokwenda hasa katika Uendeshaji wa Soka Nchini. Tanzania kama taifa tunakumbwa na Changamoto nyingi hadi kupelekea hali kuwa mbaya kuanzia ngazi ya Vilabu na hata kwa timu ya Taifa.

Watanzania wanatamani nini kwenye timu ya taifa?

Watanzania wanatamani kuiona timu yao ya taifa ikifanya Vizuri na Ikiwa tishio Barani Afrika. Watanzania wanataka siku moja Waione timu yao ikishiriki Kombe la dunia na hata kuwa washindani wakubwa; Watanzania wanataka kuona ni mazoea kwa timu yao kmushiriki michuano Mikubwa barani Afrika ya AFCON. Watanzania wanatamani timu yao itamkwe kwa Usawa sawa na Mataifa mengine kama Misri, Morocco, Algeria, Cameruni, Senegal au Nigeria.

Kikosi cha Taifa Stars

Tamaa hii haipo kwa watanzania pekee; hata Mataifa mengine yaliendelea katika soka Yalikuwa na tamaa hii miaka hiyo; Kisha Mashirikisho ya soka nchini humo yakaamua kuchukua hatua stahili zilizoyaweka mataifa hayo katika nafasi Tunazoziona kwa sasa.

Shida ya Tanzania sio Matokeo pekee;
Chini ya Kocha Emmanuel Amunike Stars ilifanikiwa Kufuzu AFCON, lakini aina ya soka walilokuwa wakilicheza lilikuwa halina kabisa Ladha na lililokosa Mpangilio maalumu, na ndio maana hata timu ilipokutana na timu zenye Mpangilio maalumu iliambulia Vipigo Mfululizo.

Kama Nchi kwanza tunakosa Mpangilio maalumu wa kiuchezaji; Kitaalamu huitwa “Falsafa” . Falsafa ni namna timu inavyojipambanua katika Usakataji Kabumbu. Hapa namaanisha Katika Vipindi Vyote Vitatu, yaani timu ikiwa na Mpira inatakiwa kuchezaje, Ikiwa haina Mpira inatakiwa kuchezaje, na katika Vipindi Vya Mpito inatakiwa kuchezaje. Timu inapokuwa katika Ukanda wa Chini inatakiwa kuchezaje, Ukanda wa kati na wa Mwisho inatakiwa kuchezaje kwa kuzingatia Vipindi Vyote Vitatu vya Mchezo.

Tanzania hatukuwa na haya mambo Kiufundi, sisi tulijua timu inatakiwa kuingia Uwanjani na Kucheza kwa kufuata maelekezo ya Kocha wao. Taifa kama taifa linapotea kama litakosa kitambulisho chake, ambacho kupitia hicho kila kitu kitaenda kuwa sawa.

Falsafa ni zao la Sera.

Katika Mpira, Falsafa huwa haiji kwa kusema mdomoni, bali inakuja katika mgongo wa kisera katika ngazi ya nchi. Hapa namaanisha Falsafa inapatikana katika kuibua, kulea na kuendeleza vipaji vya Watoto kuanzia Miaka 4 na kuendelea.

Jiulize, Katika ngazi za elimu kuanzia shule za Msingi hadi chuo kikuu kuna mashindano gani yanaendelea? Hivi michezo ya UMITASHUMTA na UMISETA bado ipo? Kama haipo tutawapata wapi wakina Dickson Job wengine?

Hivi ile Stars Maboresho nayo iliishia wapi? Kwanza ilikuwa na Lengo gani? Hivi Tanzania tuna Akademi ngapi? Na zote zinafundishwa na Makocha wa aina gani? Je huko kuna falsafa ya kueleweka au kila Akademi ina Falsafa zake?

-Maboresho

Takwimu zinaonyesha Msimu huu 2022/23 Ligi kuu Tanzania bara kuna jumla ya wachezaji 480 waliosajiliwa na kati yao 75 ni wageni ambao ni sawa na asilimia 15 pekee ya wachezaji wote. Maana yake Ligi kuu ina wachezaji 405 ambao ni Watanzania, idadi kubwa maradufu.

Jiulize; je watanzania hawa tumewakuza katika mazingira ya kufanya Vizuri kiasi cha kuifanya Ligi yetu kuwa Bora?
Kama nchi utaona tuna kazi ya kufanya ili kuhakikisha tunakuwa na wachezaji wazuri Zaidi kwa kuongeza makali ya Ligi bila kutegemea wageni, wakati huo huo Kutoka wachezaji wazuri kwa matumizi ya Timu ya taifa.

Nani ana jukumu la kujenga Falsafa ya Nchi Uwanjani?

Falsafa katika ngazi ya Taifa inaweza kutengenezwa na washirika watatu.Chama cha Soka (Shirikisho la Soka nchini).
Kule nchini Hispania, Shirikisho la soka nchini Humo linamiliki shule zake za Mpira ambazo zilianzishwa Rasmi mwaka 2008 zikianza na wanafunzi 70 na makocha Wanne (4).

Takwimu zinaonyesha mwaka 2017 tayari shule hizo zilikuwa na wanafunzi Zaidi ya 850 na makocha 40. Kazi kubwa ya shule hizi ni kuongeza thamani katika Vipaji Vya watoto, kuvilea na kuvikuza hadi kufikia kuwa “professional”.

Katika shule hizi watoto wanafundishwa hasa Vitu viwili; kwanza ni Masuala ya Kiufundi uwanjani amabyo hukuza kipaji chake na kumuongezea makali. Lakini pia kuujua Mchezo wa mpira kimbinu na kifundi; na ndio maana watafundishwa jinsi ya kuanzisha shambulizi, kumaliza shambulizi, matumizi ya Uwanja, Vipindi katika Mchezo wa Mpira, na mengine mengi ambayo huisadia timu kupata Ushindi au matokeo chanya.

Pili ni Masuala ya Intelijensia ya Mchezo. Haya ni masuala yote ya kujitambua kama Mchezaji ndani na nje ya uwanja. Hapa huhusisha masuala ya kinidhamu na Kiu ya kutaka kufanikiwa kama timu kila siku.

Tigana Lukinja (Mtangazaji wa East Africa Radio) alipokuwa nchini Ghana katika cliniki ya watoto.

Mchezaji aliyekulia katika “Academy” ni lazima awe na mambo hayo mawili kiufundi; ni lazima awe na Utambuzi Binafsi na Utambuzi wa Mchezo Mzima wa Mpira. Kuwa na Mchezaji wa aina hii, hupunguza kazi kwa benchi la Ufundi na kupelekea timu kupata matokeo kirahisi. Huku kwenye benchi la Ufundi badala ya kuwekeza nguvu kwenye Ufundi hujikuta hushughulika sana na masuala ya kinidhamu, matokeo yake ni baadhi ya wachezaji kuonekana sio Wazalendo.

Tff Kupoje?

Tff kwa sasa inasimamia kwa Ukaribu ujenzi wa Vituo viwili vya ufundi; Kimoja ni Pale Kigamboni Jijini Dar es Salaam na kingine kitakuwa kule Mkoani Tanga. Vituo hivi vitakuwa kama Academy au Shule zitakazomilikiwa na Shirikisho zenye lengo la kulea Vipaji.

Baadhi ya viongozi wa TFF wakiwa kwenye mkutano

Hii ni hatua nzuri kama Nchi katika Tasnia ya Mpira wa miguu lakini lazima nikiri kuwa ni hatua ya taratibu sana; haitoweza kuleta matokeo kwa muda mfupi, lakini kabla ya kufikia hatua hii, Shirikisho limeruka hatua moja muhimu sana. Hatua gani hiyo?
Takwimu zinaonyesha Tanzania ina makocha 21 pekee wenye Leseni ya Caf A, huku 21 wengine wakiwa na Leseni yenye Mfanano wa Caf A.

Aina hizi za makocha ndio wanatakiwa kuwa walimu wakuu katika mabenchi ya Ufundi lakini pia hata kusimamia Timu katika michuano ya Kimataifa Idadi hii ni Ndogo Mno kiasi kwamba kutokuwa na Msaada wowote katika kukuza Mchezo wa soka kama Taaluma Nchini.

Takwimu pia zinaonyesha, Ligi kuu Tanzania Bara ina Makocha wakuu Watano pekee Watanzania, huku 11 wakiwa ni wa Mataifa ya Nje. Hii tu ni dalili ya kwanza kuona kuwa kama Nchi Tuko nyuma katika Idadi ya watu wenye taaluma ya Ukocha Nchini.

Kocha Mecy Mexime, akisisitiza jambo.

Vuta picha Tanzania ingekuwa na makocha 200 tu wenye Leseni ya Caf A, unadhani Makocha wakuu wanaofundisha ndani ya lIgi wangekuwa Watano pekee? Lakini pia Unadhani hao wote wangeenda wapi? Zaidi ya kwenda kuanzisha Academy za Soka Mtaani?
Ujerumani miongoni mwa mbinu walizozitumia kupata aina ya Mpira wanaoutaka kama alama ya nchi yao ni Kutoa nafasi nyingi Zaidi za Kufadhili Kozi za Ukocha na kutoa nafasi kwa Wajerumani wengi Kuwa wakufuzi wa Soka. walipoona kama nchi wana idadi nzuri ya wakufunzi wa soka, Mwaka 2002 wakaanzisha Programu wakaiita “ Extended Talent Promotion Program”.

Kupitia Programu hiyo, Ujerumani ikafungua Vituo 366 nchi nzima, ambapo vipaji vilivyoibuliwa vililelewa na kuibuliwa na hata kuwa wachezaji muhimu kwa taifa.
Mafanikio hayo hayakuja kwa bahati mbaya, kwanza yalianzia kwa makocha ambapo hadi sasa ninapoandika Uchambuzi huu Ujerumani ina Zaidi ya makocha 28,500.

TFF Kwanza izalishe makocha wengi, kisha iweke mazingira mazuri ya kuanzisha Vituo vya kukuzia na kulelea Vipaji vya Mpira, kisha wafuatilie katika mlengo wa kifalsafa na aina ya soka wanalolitaka Lifundishwe kwa nchi nzima. Kufanya hivi kuna Faida kuu mbili; kwanza wachezaji watakulia academy, pili ni Nchi itakuwa na Falsafa ya kueleweka, kitu ambacho kitaleta matokeo chanya katika timu yetu ya Taifa.

Hilo moja; Pili TFF bado haijatilia Mkazo sana kwenye mashindano ya Vijana.

Sheria inazitaka timu zote zinazoshiriki ligi kuu Tanzania bara kuwa na timu ya Vijana. Lakini timu hiyo ya Vijana haina mashindano makubwa wala ya Muda mrefu inayoshiriki. Maana yake Timu zinamiliki timu za Vijana kwa sababu tu ya sheria lakini kiuhalisia hazina faida yoyote Zaidi ya kutia hasara Klabu.

Huwezi kuwa na Falsafa kama hutaki kuwekeza Kwenye soka la Vijana. TFF inatakiwa kuja na Ligi ya Vijana ambayo itaenda sambamba na ligi ya wakubwa. Hii itawafanya Vijana kuwa vizuri muda mwingi, lakini pia kumbuka hao ndio hazina ya nchi.

Timu za Mpira

Vilabi kama Simba, Yanga na Azam ndio Vilabu vikuu na ndio vinavyotoa wachezaji wengi katika timu ya taifa. Vilabu hivi vitatu visipoeleka Kiufundi athari yake itaangukia hadi kwenye timu ya Taifa. Vilabu hivi ni lazima viwe na Utaratibu maalumu na jiNsi vinavyojiendesha.

Kwa Mfano Simba; Miaka ya hivi karibu imepitia katika hali ambayo haina afya katika kudumisha na kuendeleza falsafa yake kiuchezaji kutokana na timua timua za makocha, huku Klabu ikileta Kocha anayefundisha Falsafa Nyingine ile iyopo.
Simba hadi sasa haina nafasi moja muhimu kiutendaji “ Mkurugenzi wa Ufundi”.

Mkurugenzi wa Ufundi ana kazi nyingi lakini mojawapo ni Kusimamia Falsafa ya Klabu bila kusahau Tamaduni Zake. Hapa ndipo kunachangamoto inayoitafuta Simba hadi sasa. Kivipi?
Baada ya kuachana na Didier Gomes Da Rossa, Wakampata Muhispania Pablo Franco Martine kama Kocha Mkuu kisha akafundisha Falsafa Nyingine tofauti na Ile Falsafa Mama ya klabu; Klabu ingekuwa na Mkurugenzi wa Ufundi mwenye mamlaka Kamili; Pablo asingetambulisha Falsafa yake Mpya kwa Klabu; Haiwezekani, Simba B ifundishe Falsafa Nyingine, huku Simba A nayo ifundishwe Falsafa Nyingine; Maana yake Ule Mnyororo wa Wachezaji kutoka Timu B kupandishwa Timu ya Wakubwa Unakatwa; Na Ukikatwa Timu itakuwa inategemea Kununua tu; Kitu ambacho sio Biashara ni Hasara.

Kwa bahati nzuri wakamtimua kabla ya Kufanya Usajili; Wangemuacha, angesajili wachezaji 12-15 watakaofiti katika Falsafa Yake, lakini Pia Ndio kipindi pekee kwa Wachezaji wengi na Muhimu wa Klabu kuonekana kushindwa Kufiti katika Mipango ya Kocha.

Hawakuishia hapo Wakamleta Zoran Maki bila kuzingatia ishu ya Falsafa; wakajikuta wanasajili Bila kujua Kocha atahitaji aina gani ya wachezaji; Kilichotokea ni ile Migogoro ya Kiufundi ya akina Akpan, Mara Onyango, Mara Mkude. Shida ilianzia hapa; Kukosekana Kwa Mkurugenzi wa Ufundi ambaye angesajili kutokana na Falsafa ya Klabu kisha kuleta kocha anaendana na Falsafa iliyopo.

Kama Nchi hasa Shirikisho la Soka Nchini lazima liwe na Ushawishi kwa Vilabu hivi, lakini pia lazima lije na sheria za kiuendeshaji zitakazozilazimisha Klabu zote kuwa na walezi wa Kifalsafa na Tamaduni za Klabu kama Mkurugenzi wa ufundi.

Hilo Moja, lakini pili, Vilabu vyetu bado havijui jinsi Mpira unavyoweza kuendeshwa kama Biashara. Sio Simba, sio Yanga, hawana Biashara kubwa wanayoifanya kwenye Mpira Zaidi ya Wadhamini, haki za matangazo, Viingilio na Mauzo ya Jezi. Timu hizi hazifanyi kabisa biashara ya Uuzaji wa Wachezaji, zenyewe kazi yao ni kununua tu kila msimu na ndio maana tazama idadi ya wachezaji waliowapandisha kutoka timu zao za Vijana Msimu huu.

Kama Vilabu Vikubwa kama hivi havina Vijana kwenye timu zao maana yake hakuna Msingi Mzuri wa kimalezi katika Academy za Klabu nchini. Ni muda wa kuchukua hatua stahiki sasa.

Serikali.

Serikali ndio kila kitu katika hili. Serikali ina nguvu za kutengeneza sera na kisha kuzitekeleza. Serikali inaweza andaa mazingira mazuri kwa kufunguliwa kwa Acadeny nyingi Zaidi lakini pia ikatenga maeneo mengi ya wazi kwa ajili kufanyikia shughuli mbalimbali za michezo.


Lakini pia Bila shaka Unajua, Jukumu la timu ya Taifa ni Jukumu la Serikali. Serikali haitakiwi kuishia juu, yaani haitakiwi kutoa pesa za safari, kambi na maandalizi ya mechi kwa timu ya taifa, lakini inatakiwa kuhusika moja kwa moja kuanzia katika hatua ya awali kabisa hadi kuipata timu ya Taifa Bora.
Hatua ya awali kwa serikali ni kuibua Vipaji huko Mashuleni, kisha Kuvilea na kuviendeleza.

MH. Mchengerwa (Kulia), Waziri na Mh. Abbas (Katibu Mkuu). Wizara inayohusika na michezo)

Michezo kama ya Umitashumta na Umiseta ianze Upya, lakini pia lazima kuwekwe mazingira rahisi kwa watu kufungaua Vituo vya kuibua, kulea na kukuzia Vipaji Mtaani. Kufanya hivyo ni Kuwatengenezea njia nzuri wachezaji toka wakiwa wadogo hadi kuja kuitumikia timu ya Taifa.


Kama Taifa, tukitaka kuwa na matokeo chanya kwenye timu zetu za taifa ni lazima tukubali kuwa na alama moja inayotuwakilisha Kicuhezaji. Alama hiyo ni Falsafa, na falsafa huanza kuumbwa kutoka soka la Watoto katika vituo vya kuibua, kulea na kukuza Vipaji.

Wingi wa Vituo Hivi ndio chanzo cha Falsafa Husika kutawala hata kuleta matokeo chanya kwa taifa. Falsafa ndio Nyenzo ya timu bora ya taifa, Ukizingatia timu za taifa huwa hazikai kambi kwa muda mrefu hivyo ni ngumu sana kuwa na mpira nzuri timu ikiundwa na Wachezaji wanaotoka kwenye klabu zenye Falsafa mbalimbali. Nchi ikiwa na falsafa Moja inayoeleweka, Benchi la Ufundi hutumia muda mfupi sana kutengeneza timu yenye Makali.

Haya yote hayaji kwa Siku Moja, bali huchukua muda. Kama taifa lazima tukubali maumivu ya kuwekeza ili kupata matokeo chanya kwa siku za Usoni.

Sambaza....