Kariakoo Derby kwa mara nyingine tena inawakutanisha Yanga Sc dhidi ya watani wao Simba Sc
Ni mechi kubwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na ambayo umejizolea umaarufu mkubwa sana tangu kuanzishwa kwa vilabu hivi viwili vya jijini Dar es salaam.
Kwenye mechi ya ngao ya jamii msimu uliopiga Yanga iliifunga Simba bao moja kwa moja kwa bila, goli la Fiston Mayele. Tangu hapo Yanga ikawa na msimu mzuri wa mashindano na kufanikiwa kubeba kombe la ligi kuu, shirikisho pamoja na ngao ya jamii.
Jumamosi hii nyasi za uwanja wa Mkapa zitakuwa kwenye wakati mgumu pale ambapo wachezaji wa Yanga na Simba watashuka hapo kuchanga karata zao kwa msimu mpya.
Mechi hii itakuwa na mvuto kutokana na usajili ambao kila timu imefanya msimu huu, Yanga wameongeza wachezaji kwenye eneo la kati, huku pia wakiboresha eneo la ulinzi kwa kusajili beki wa kushoto Lomalisa ambaye ana uzoefu wa kucheza ligi kubwa barani Ulaya (Ligi ya Ubelgiji) eneo la kati Yanga imeongeza mtu mwenye CV kubwa sana kwenye soka la Ulaya, huyu ni Gael Bigirimana.
Morrison, Aziz Ki, Lazarous Kambole wote hawa wanategemewa kuleta ugumu kwenye safu ya ulinzi ya Simba ambayo pia imesajili beki kutoka Ivory Coast Mohamed Quattara aliyekuwa akikipiga Sudan na klabu ya Al Hilal.
Nelson Okwa, Augustine Okrah, Victor Akpan, Dejan Georgijovic, Habib Kyombo wote hawa ni wachezaji wapya wenye uwezo mkubwa ambao pia wanategemewa na Simba kwenye kuanzisha mashambulizi na kumalizia mashambulizi yao.
Nelson Okwa na Augustine Okrah wote hawa wamecheza kwenye mechi ya Simba Day dhidi ya St. George ya Ethiopia na wameonekana kuwa na kasi kwenye kushambulia hivyo beki za Yanga lazima ziwe kwenye umakini wa muda wote kuhakikisha wanazuia nyota hao.
Ni Derby kubwa na Derby yenye wachezaji wapya ambao wanataka kuonesha kuwa hawakusajiliwa kwa bahati mbaya na vilabu vyao.