Michuano ya AzamSports Federation Cup inakaribia kufikia tamati ambapo July 2 mwaka huu itafikia tamati katika dimba la Sheikh Amri Abeid katika Jiji la Kitalii Arusha.
Ili fainali ya michuano hii itimie ni wazi lazime awepo wa kuungana na Yanga ambapo mshindi mmoja kati ya Coastal Union na Azam ndie atakayeungana nae kucheza mchezo wa fainali.
Tuhamie huku kwenye vita ya Wagosi wa Kaya Coastal Union dhidi ya Azam Fc katika nusu fainali ya pili itakayopigwa katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid kesho mchana.
Coastal Union ni kama wamefufuka hivi baada ya urejeo wa Juma Mgunda “Guardiola mnene” akichukua kiti cha Melis Medo alietimuliwa kutokana na matokeo mabovu klabuni hapo. Katika michezo mitano ya mwisho Coastal Union imepata ushindi michezo minne na mmoja pekee wakitoa sare.
Coastal imefikia hatua ya nusu fainali ya FA kwa mara ya kwanza tangu michuano hiyo ibadilishe jina na kuanza tena katika msimu wa 2015/2016. Imefika hatua hii baada ya kuwaondosha Mtibwa Sugar.
Kwa upande wa Azam Fc wao ni kama bado hawaeleweki, licha ya kuanza vyema kocha Moalin aliechukua mikoba ya Lwandamina lakini sasa kikosi cha Azam kimekua na matokeo ya kusuasua katika Ligi.
Ni mchezo utakaowakutanisha wakubwa katika nchi hii, ukiwaondoa Simba na Yanga ni wazi Coastal Union na Azam Fc ni miongoni mwa vilabu vinavyofwatia kwa kuwa na mashabiki wengi.
” The Mangush” Coastal Union wao ni kama wapo nyumbani tuu maana safari ya kutoka Tanga mpaka Arusha ni mwendo wa masaa matatu mpaka manne hivyo Sheikh Amri Abeid itajazwa na rangi nyekundu na nyeupe.
Tusubiri tuone ni nani ataungana na Yanga katika fainali ya FA itakayopigwa mkoani Arusha pia July 02.