Kwanini Haruna Moshi Boban
Hakuyapenda Maisha Ya Ulaya…? Ni swali ambalo Maggid Mjengwa, moja ya mwandishi mahiri hapa Tanzania ameuliza. Tovuti ya kandanda katika pita pita zake mitandaoni ilikutana na hii stori tunadhani ni muafaka kuiweka katika maktaba hii kubwa Tanzania ya makala zinazohusu Kandanda.
Endelea kusoma jibu lake kama alivyoandika Mwenyekiti mwenyewe.
Yumkini Haruna Moshi alishawishiwa kutokukipenda ambacho kingemsaidia maishani.
Siamini kama Haruna Moshi hakuyapenda maisha ya Ulaya. Kwamba inatajwa kuwa ni moja ya sababu kubwa iliyochangia Haruna Moshi kukatisha mkataba wake na klabu ya Gefle IF ya Sweden.
Nilipata kufika Mji wa Gavle, Sweden. Ni mwaka ule wa 2010. Nikapata hata kuyasikia ya wenyeji wa Haruna Moshi na kwa lugha yao ya Kiswidi.
Kwa mujibu wa kocha wa Gafle If , Pelle Olson, Haruna Moshi alikuwa na uwezo wa kuchukua namba klabuni hapo kutokana na uwezo wake mkubwa wa kusakata kandanda.
Ilifika mahali uongozi wa Gafle If ulitengeneza clip maalum ya Haruna Moshi na kuiweka mtandaoni. Lengo lilikuwa kumwingiza Haruna Moshi sokoni.
Uongozi wa Gafle If uliamini Haruna Moshi hakuwa wa kiwango cha kucheza Ligi ya Sweden. Kwamba wangeweza kumuuza kwa fedha nyingi kwenye moja ya vilabu vikubwa vya Ulaya.
Lakini, mazingira ya nje ya uwanja yalikuwa ni kikwazo kikubwa kwa Haruna Moshi. Ni pamoja na ya nyumbani Tanzania.
Kwenye kikundi kile cha ‘ Marafiki wa Lunyasi’ walitamani kumrudisha Haruna nyumbani Bongo kwa maslahi yao tu. Hivyo, mmoja wa ‘ Marafiki wa Lunyasi’ alifanikiwa kumchota Haruna Moshi kiakili.
Ni kawaida kwa wenzetu wa Ulaya kutosema kila kitu kuhusiana na mchezaji walieingia naye mkataba, hususan inapohusu masuala binafsi. Ni jambo la kiungwana.
Na makala haya pia yanazingatia uungwana huo. Tunaandika haya kwa uchache iwe kama elimu tu kwa vijana wenye malengo ya kucheza kandanda Ulaya. Kwamba wanahitaji kujiandaa, na zaidi, shule za soka zitumike. ( Football academies.)
Kimsingi, Haruna Moshi ni kielelezo cha tatizo linalowakuta wachezaji wetu wanaopata nafasi ya kucheza soka Ulaya. Inahusu zaidi maandalizi ya kisaikolojia pamoja na kujifunza namna ya kuwasiliana vema na kocha na wachezaji wengine klabuni.
Inahusu pia ufahamu wa utamaduni wa nchi ambayo mchezaji anakwenda kucheza. Tuchukulie tena mfano wa Haruna Moshi. Simulizi nzima juu ya yeye kufikia hatua ya kukatisha mkataba wake inanipa picha ya mtu aliyekuwa ‘ bored’ ( aliyechoshwa) na aliyekuwa akikumbuka nyumbani.
Hivyo, ikawa rahisi kwake kutamanishwa na kauli za kiongozi wa soka wa nyumbani aliyefikia hata kumpa mbinu Haruna za kuvunja mkataba, badala ya kumtia moyo wa kupambana ili afike mbali zaidi.
Maana, Klabu ya Gefle If ilimpa Haruna Moshi, mbali ya mshahara mzuri sana kwa viwango vya Bongo, ikampa pia yote muhimu aliyohitaji ikiwamo nyumba ya kuishi katikati ya mji wa Gavle.
Ni Tafakuri Jadidi.
Maggid Mjengwa.