Ukilitazama vizuri benchi la ufundi la Simba lina mtu kama Sven Vandenbroeck ambaye ni Kocha Mkuu, Kuna Selemani Matola ambaye ni kocha Msaidizi, pia kuna Patrick Rweyemamu kama meneja wa Timu kuna Adel Zrane kama kocha wa Viungo, Muharami Sultan kama Kocha wa Makipa,Yassin Gembe kama daktari wa Timu huku Paul Gomez na Jallow Bakari kama Madaktari wa Viungo.
Kati ya hao wote kuna mmoja ni Mjerumani na aliongezwa na klabu kipindi kile Simba ikiwa kambini nchini Afrika Kusini chini ya Kocha Patrick Aussems.
Huyu anaitwa Paul Gomez, kifani ni Daktari wa Viungo wa Mabingwa wa nchi . Hadi sasa Gomez amefikisha msimu mmoja tangu ajiunge na mabingwa hao wa nchi, lakini maswali bado ni mengi…
Huenda unajiuliza, hivi jamaa kazi yake ni nini pale Simba? Kwani amefanya kipi cha maana hadi sasa? Ameisadiaje klabu kufikia mafanikio yaliyopo sasa? Majibu yote yako hapa.
Gomez ni tofauti na Zrane, Zrane ni Kocha, huku Gomez ni Daktari. Gomez ni daktari wa Mazoezi ya Viungo. Hii inamaanisha kuwa Gomez Ni Mtaalamu wa kuzuia Majeraha kwa Wachezaji pindi wanapokuwa dimbani kuanzia mazoezini hadi kwenye Mechi kwa kuzingatia matumizi yao kwa uhusiano wa miaka na uwezo wao.
Gomez ni Mshauri juu ya matumizi ya mchezaji Fulani kulingani na hali yake kiafya na hata umri wake. Huyu jukumu lake kubwa ni kuwasaidia wachezaji kubaki katika kiwango kizuri katika muda wote wa Msimu na kuzuia majeraha kwa wachezaji.
Gomez husimamia mazoezi ya Mchezaji mmoja mmoja wakiwa Kliniki ya Tiba ya mazoezi kulingana na tatizo la mchezaji husika, pia anaweza kuhudhuria katika mazoezi ya klabu, huyu hutoa matokeo ya kiafya kwa wachezaji na utimamu wao, pia ndiye mtoa Masomo juu ya jinsi ya kujizuia na majeraha kwa wachezaji wawapo dimbani.
Tukiachana na majukumu haya ya kiujumla, Acha tukamtazame Gomez huku tukimlinganisha na majukumu yake ndani ya Simba.
Ndani ya Simba Gomez ni Meneja wa Wachezaji wenye Majeraha.
Katika hili Gomez ndiye mtu wa kwanza kuzuia ongezeko kubwa la idadi ya wachezaji Majeruhi ndani ya Simba. Kazi yake ni kutambua hatari ya mchezaji kupata majeraha katika mchezo au mashindano kutokana na kiwango cha afya yake kabla ya mechi. Mfano, Luis Miquissone, Kahata, Paschal Wawa na wengine walishindwa kucheza mechi dhidi ya Vitalo na Namungo kwa sababu tu hawakuwa fiti na kama wangecheza basi kungekuwa na hatari kubwa kwa wao kupata majeraha.
Wawa alipoumia kwenye mechi ya Klabu Bingwa
Lakini pia mbali na jukumu hili, Gomez anatakiwa kumshughulikia mchezaji haraka iwekanavyo baada ya kupata majeraha, kuanzia uwanjani wakati wa mazoezi, mechi na hata nje ya uwanja. Ndio maana Mchezaji wa Simba akiumia uwanjani, Yassin Gembe huongozana na Gomez na kumshughulikia. Gomez ndio ndio jukumu lake hilo…
Katika jukumu la kuzuia Majeruhi kwa Wachezaji, Gomez hutumika kutambua majeraha yasiyoonekana kwa mchezaji. Hapa kazi yake huwa ni kuwapima wachezaji na kubaini matatizo yao kiafya, na kujua jinsi ya kutatua matatizo hayo.
Hivi unajua mchezaji anaweza kumaliza mechi, kwa nje akaonekana hajaumia lakini kumbe anajeraha hatarishi? Nani kulitambua jeraha hili lisiloonekana? Ni Gomez pale Simba.
Lakini pia Gomes anaweza kumuingilia kocha Mkuu juu ya matumizi ya Mchezaji Fulani kulingana na hali yake kiafya, hata utimamu wake katika mechi. Gomez ndio hutoa majibu, Mchezaji Fulani anatakiwa acheze dakika ngapi uwanjani kulingana na hali yake.
Pili Gomes ndani ya Simba ni Mshauri.
Gomez ndio hushauri mfumo mzuri wa maisha kwa wachezaji wa Simba ili kuimarisha utimamu wao kiafya na uwanjani. Gomez hufanya kazi bega kwa began a Daktari wa timu, kocha wa viungo na kocha mkuu hasa katika matumizi sahihi ya Dawa na Mazoezi.
Simba Mazoezini
Ulishawahi kusikia Mchezaji amepewa dawa za kupona haraka ili aiwahi mechi Fulani? Gomez kazi yake ni kushauri matumizi sahihi ya madawa kwa matumizi halali na sahihi kwa mchezaji ili kulinda afya na kiwango chake kwa siku za mbeleni.
Tatu, Gomez ndani ya Simba ni Kiongozi Mtaalamu.
Hapa kazi yake kubwa ni kuhakikisha ubora wa utoaji wa huduma unakuwa mkubwa kwa siku zote. Yeye ndiye wa kuhakikisha Upimwaji wa wachezaji mara kwa mara, na vifaa vya msingi vinavyotumika vinakuwa katika usalama na ubora wenye vigezo vinavyohitajika.
Lakini pia Udaktari wa Viungo maana yake ni kuwa vizuri katika matumizi mazuri ya muda, rasilimali na watu, na haya yote hutimizwa kwa njia ya kitaalamu zaidi na kuzingatia maadili ya kazi.
Nne, Gomez ni Mvumbuzi.
Hapa kazi yake ni kila siku kufanya utafiti na ubunifu katika tasnia hii ya matibabu ya viungo. Gomez anahitajika kuendana na maendeleo ya dunia kuhakikisha anakuwa vizuri, anawatibu wachezaji kwa njia za kisasa ili wapone haraka zaidi, lakini pia anatakiwa kuwa na mawasiliano na Wataalamu wenzake kote duniani ili kupeana mbinu zaidi za matibabu kwa wachezaji.
Mbali na majukumu haya yote, lakin I ukimuuliza mchezaji yeyote yule duniani nini faida ya kuwa na Daktari wa viungo? Yeye atakwambia kuwa Daktari wa Viungo anasaidia kuzuia majeraha kwa wachezaji na pia huwasaidia wachezaji kupona haraka.
Kwa kuzingatia Majukumu haya mawili, acha tumchimbe Gomez wa Simba ili kujua kama atakuwa amefanikiwa au amefeli ndani ya Msimu wake mmoja..
1. Kuzuia Majeraha.
Gomez alijiunga na Simba mwezi July mwaka 2019, timu ikiwa kambini nchin Afrika ya Kusini kujiandaa na msimu mpya wa ligi Tanzania bara na klabu bingwa Afrika.
John Bocco (c)
Wakati Gomez akiwa bado mpya Mpya, John Bocco alipata majeraha, Gomez alishindwa kumtibu, ikabidi Simba wampeleke Nchini Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu zaidi.
Bado Hajakaa sawa, Mshambuliaji wa Kibrazil Henrique Da Silva naye anapata majeraha. Majeraha yake yalichukua miezi kadhaa kabla ya kupona na kuingia uwanjani tena.
Mwezi Novemba mwaka 2019, Shomari Kapombe naye anaumia akiwa na timu ya taifa.. Gomez alishindwa pia kumtibu, Ikabidi Simba impeleke Afrika ya kusini kwa matibabu zaidi..
Majeraha haya ndio sababu ya Simba kutolewa mapema, katika hatua ya awali klabu bingwa Afrika dhidi ya UD Do Songo ya Msumbiji, Kwani Aussems alilazimika kumtumia Mshambuliaji Mmoja tu.
2. Wachezaji kupona haraka Majeraha.
Msimu uliopita Mchezaji john Bocco alikaa sana nje kwa ajili ya Majeraha, Miraji Athumani bado hajawa fiti hadi leo kutokana na kusumbuliwa na majeraha, Miraji amekaa nje ya uwanja kwa zaidi ya miezi miwili, Deo Kanda naye amesota muda mrefu kuipambania afya yake.
Miraji Athuman
Mejeraha mengi kwa wachezaji wa Simba yameonekana kuchukua muda mrefu sana, kana kwamba timu haina Paul Gomez.
Rekodi zinaonyesha kuwa, Gomez amefanikiwa kwa majeraha ya pili ya Kapombe, baada ya kuumia katika mechi dhidi ya Azam, ikiwa ni siku chache kabla ya kuvaana na yanga katika mchezo wa nusu fainali Azam Sports Fedaration Cup.
Wengi hawakutazamia, Kapombe aliingia dimbani na kucheza vizuri, hii ndio kazi pekee inayompa sifa Mjerumani Paul Gomez.
Lakini hata hivyo, hatutakiwi kumlaumu Gomez kwa kushindwa kuwatibu wachezaji wa Simba haraka, Sababu huenda ni nyingi ikiwemo kukosekana kwa vifaa vya matibabu.
Mbali na Masuala ya Matibabu, kuna masuala ya ushauri kwa benchi la Ufundi juu ya matumizi ya mchezaji Fulani kulingana na hali yake kiafya au umri.
Miongoni mwa kazi za Gomez tumeona ni kulishauri benchi la ufundi chini ya Sven hasa juu ya matumizi sahihi ya wachezaji wenye Umri kuanzia miaka 30 na kuendelea ili kulinda viwango vyao na hatari ya kupata majeraha.
Kwa maelezo haya bila shaka utakuja na jibu moja sahihi kati ya haya, Simba imtafute Daktari mwingine wa Viungo imtimue Gomez au Imuache aendelee kuihudumia Simba? Kumbuka malengo ya Simba MSIMU HUU NI KUFIKA HATUA YA MAKUNDI KLABU BINGWA AFRIKA.