IMEFAHAMIKA kuwa wadhamini wa Yanga ambao ni Kampuni ya GSM, wametumia gharama kubwa kwenye usajili katika msimu huu kwa kutumia kitita cha Sh bilioni 1.09 huku watani wao Simba walio chini ya bilionea, Mohamed Dewji ‘Mo’ wakitumia Sh 678 Mil.
Yanga imetumia fedha hizo kwa kuwasajili wachezaji kumi pekee wapya katika kuelekea msimu ujao huku ikiendelea na usajili wake huku Simba wenyewe ikiwasajili nyota wake saba.
Simba wenyewe tayari usajili wa wachezaji wao wapya wamefunga huku Yanga ikiahidi kuendelea kushusha vifaa vipya, kati ya hivyo yupo kiungo mshambuliaji anayekipiga Klabu ya Interclube ya nchini Angola, Carlos St’enio Fernandez maarufu kwa jina la Carlinhos.
Tetesi zinaeleza kuwa, Carlinhos anatarajiwa kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam leo Jumatatu tayari kwa ajili ya kusaini mkataba na kuanza maandalizi ya msimu mpya.
Yanga imetumia gharama hizo kwa kuwasajili Tuisila Kisanda (Sh 230Mil), Mukoko Tonombe (Sh 230 Mil), Michael Sarpong (120 Mil), Bakari Mwamnyeto (220 Mil), Yacoub Sogne (100 Mil).
Wengine ni Zawadi Mauya (30 Mil), Farid Mussa (70 Mil), Wazir Junior (30 Mil), Kibwana Shomari (30 Mil) na Yassin Mustapha (30 Mil). Jumla ni Sh bilioni moja na milioni 90.
Kwa upande wa Simba wachezaji waliowasajili ni Chris Mugalu Sh 140 Mil, Larry Bwalya (138 Mil), Joash Onyango (80 Mil), Ame Ibrahim (30 Mil), Charles Ilanfya (30 Mil), Bernard Morrison (230 Mil) na David Kameta (30 Mil). Jumla Sh mil 678.
Yanga imeonekana kutumia gharama kubwa kwenye usajili kutokana na baadhi ya wachezaji kuivunja mikataba yao kwenye klabu zao zilizokuwa zinawamiliki.
Kati ya wachezaji hao mikataba yao iliyovunjwa ni Tuisila, Tonombe waliokuwa wanaichezea AS Vita na Bakari Mwamnyeto aliyekuwa anamilikiwa na Coastal Union ya mkoani Tanga.
Mkurugenzi Mwekezaji wa GSM, Injinia Hersi Said, hivi karibuni alisema: “Usajili tulioufanya ni wa kibiashara na malengo kwa klabu kwa kuhakikisha tunafanya usajili ulio bora na wa kisasa.
“Hiyo ndiyo sababu ya kutumia gharama kubwa kusajili wachezaji kwa gharama kubwa kuvunja mikataba kwenye klabu zao wanazozichezea, mfano usajili wa Tonombe na Tuisila haukuwa rahisi, hiyo ni kutokana na wachezaji wenyewe kuwa na mikataba mirefu.
“Hivyo tukalazimika kutumia gharama kubwa kuvunja mikataba yao ili kuhakikisha wanakuja kuichezea Yanga na kikubwa ni kuona timu yetu tunauchukua ubingwa wa msimu ujao.”