Jogoo zito la kushiba ndilo lilokuwa likimuamsha Tigana mtoto wa mwisho yaani kitinda mimba katika familia ya Mzee Lukinja katika kijiji cha Uwemba mkoani Iringa, sasa ni Mkoa wa Njombe. Uwemba inawanisionari Wabenenektini kutoka Kanisa Katoliki, hapo kuna kanisa kubwa.
Asubuhi hiyo baada ya jogoo kuwika alitakiwa kufuata au kuteka maji kisimani ‘Uve Tigana tegule iligaloni uhanege ululenga huhisima, hadza upilwihe unfyagilage uluvanja”. Sauti ya Mama Sangunagwa hiyo ikimuamsha akimaanisha Tigana aamke akachote maji kisimani na akirudi afagie uwanja wa nyumba.
Amadou Jean Tigana ni mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Ufaransa, akicheza katika nafasi ya kiungo. Alicheza soka lake la kiushindani katika nchi ya Ufaransa akicheza mechi takribani 52 katika timu ya taifa na kufunga bao moja.
Huyo ni Tigana ambaye ulimwengu unamfahamu zaidi, hapa kwetu Tanzania tumekuwa na wachezaji wawili ambao walifahamika kwa majina hayo hayo, Ally Yusuf ‘Tigana’ na Tigana Lukinja. Mtandao wetu sasa leo haujaenda kule kijijini kwake anakoteka maji ‘kwivindi’, tumemfuata mitaa ya Kimara tu hapa hapa Jijini Dar es Salaam, wenyewe wanaita ‘Kubomaa’.
Mpwa Tigana au Ticha Tigana kama wanavyomuita, jina lake Tigana si kwasababu ya Amadou Jean Tigana, na kumbuka si kwasababu ya Ally Yusuf ‘Tigana’. La hasha, hili ni jina lenye asili ya Kibena likimaanisha ‘Fanya Bidii’ au ‘Kazana’ vijana wa mjini wangesema ‘Pambana’. Katika familia yake hakika ni ‘Tigana, maana yeye ni kitinda mimba katika familia ya watoto wanne walio hai akiwa na Dada mmoja na kaka wawili. Tigana huyu akizaliwa Ubenani huko wakati Tigana yule Mfaransa akizaliwa Bamako, Mali (France Sudani enzi hizo), Baba yake akiwa ni Mmali na Mamayake akiwa Mfaransa.
“Mpira wa miguu ‘Kabumbu kunoga’ kwangu ulikuwa ni kila kitu, na nilikuwa nawaza mbali sana kwaajili ya mpira huu huu ninaouangalia kwa jicho la kiufundi siku hizi.” Tigana alianza kuongea na Mtandao huu.
Mpira wa miguu ulianza kumtafuta rasmi Tigana pale Changanyikeni Rangers ambayo ipo maeneo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Hapo pakiwa ni mtaani kwake wakati wakiishi jiji Dar es salaam, timu hiyo ilianzishwa na vijana waliokulia mitaa hiyo baada ya kuonyesha vipaji vikubwa sana. Changanyikeni Rangers hivi sasa ipo daraja la pili ngazi ya taifa.
Wanasoka magwiji duniani wananjia tofauti jinsi wanavyoingia katika soka, kwa upande wa Afrika huwa hatutaji sana Shule za Soka, bali mtaani ndiko tunakopata elimu ya mpira huu maarufu duniani.
Nini kilifuata baada ya hapo? je ali’tigana’ kiasi gani? Subiria sehemu ya pili kujua mchakato wa mpira kumchukua hadi Ligi Kuu humuhumu katika mtanda pendwa wa www.kandanda.co.tz.