Kiungo Feisal Salum “Fei Toto” ni kama alikua amesahaulika hivi katika kikosi cha Yanga baada ya kukosa nafasi hata ya kukaa benchi katika michezo ya Yanga ya hivi karibuni katika Ligi Kuu Bara na FA.
Mwalimu Luc wa Yanga amekua akiwatumia Niyonzima, Balama Mapinduzi, Papy Tshishimbi na Mo Banka katika eneo la kiungo la Yanga na hivyo Feisal kukosa kabisa nafasi katika kikosi cha kwanza Yanga.
Lakini katika mchezo uliopita wa Ligi kati ya Yanga na Alliance Feisal alipata nafasi ya kuanza na kuonyesha kua bado yumo huku akichangia kwa kiasi kikubwa ushindi wa mabao mawili wa Yanga.
Mwalimu Luc mwenyewe alikiri kua Feisal ameimarika mazoezini na kwenye mechi na hivyo kuonekana yupo kwenye mipango yake katika mchezo wa Derby March 8 ambao Yanga ndio wenyeji wa mchezo huo.
Luc Aymael alinukuliwa akisema “Feisal ni mchezaji mzuri sana na ana kipaji kikubwa pia, ukimuangalia mazoezini basi utamgundua ni mchezaji wa aina gani, kuna vitu vidogo sana vilikuwa vinamfanya ashindwe kufanya vizuri, nadhani kwa sasa vimemalizika na unaona jinsi ambavyo amecheza vizuri, hakika natamani acheze hivi kila siku,”
Ama kwa hakika kwa Feisal amefufuka wakati muafaka haswa katika kulekea mchezo dhidi ya Simba na hivyo kumpa mwalimu uchaguzi mwingi katika eneo la kiungo.
Tangu kuondoka kwa kocha Mwinyi Zahera Feisal amekua kama amesahaulika hivi na Mwalimu mpya wa Yanga Luc Aymael, lakini pia mpango wa kwenda Misri kwenye majaribio kufeli pia ni kama ulimtoa mchezoni.
Feisal anakua tumaini jingine kwa Wanayanga katika eneo la kiungo na kutengeneza muunganiko mzuri kati yake na viungo wengine kina Niyonzima Mapinduzi na Tshishimbi ili kuweza kuwadhibiti kina Mkude, Chama, Kahata na Miquissone wa Simba.